Obama atoa hotuba ya mwisho kuhusu hali ya Taifa la Marekani
13 Januari 2016Rais Obama amewataja wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu IS kama wauaji wenye misimamo mikali ambao wanastahili kusakwa na kuangamizwa na kulitaka bunge la Marekani kuidhinisha matumizi ya nguvu za kijeshi kulikabili kundi hilo la IS akisema hata hivyo kwamba vita hivyo havitakuwa vita vya tatu vikuu vya dunia.
Obama amewataka Wamerakani ambao wanatiwa wasiwasi na kitisho cha ugaidi na hali ya kiuchumi kutohofu na badala yake wanahitaji kufanya maamuzi kati ya kuogopa mabadiliko au kuzikabili siku za usoni kwa ujasiri.
Katika matamshi yaliyoonekana kuwashutumu wagombea Urais wa chama cha Republican ambao wamekuwa wakiukosoa utawala wake kuhusu jinsi ilivyoshughulikia sera za kigeni na uchumi, Obama amesema Marekani imepitia nyakati ngumu katika kipindi cha nyuma na ni wakati wa kufanya mabadiliko ya kipekee ili kusonga mbele akiongeza kuwa madai kuwa uchumi unasusua ni uongo.
Ni wakati wa kukubali mabadiliko
Kiongozi huyo ambayehuu ni mwaka wake wa mwisho madarakani, amewataka wabunge wa taifa hilo kushughulikia masuala makubwa yanayoikabili nchi hiyo bila ya kuzingatia ni nani atakuwa Rais baada yake ikiwemo jinsi ya kutoa fursa za kiuchumi, kuimarisha teknolojia ili kuinua maisha ya watu, namna ya kuifanya Marekani kuwa salama na kuimarisha mazingira ya kisiasa nchini humo.
Kuhusu sera yake ya kigeni Obama ameonekana kutetea mtizamo wake wa kutumia ushirikiano na washirika wengine kupitia juhudi za kidiplomasia badala ya kutumia zaidi nguvu za kijeshi.
Obama pia amesema Makamu wake Joe Biden ataongoza juhudi mpya za kuifanya Marekani kuwa taifa linaloweza kutibu kikamilifu saratani. Kiongozi huyo wa Marekani ambaye anamaliza muhula wake wa pili madarakani mwaka huu, pia amelitaka bunge kuliondolea vikwazo Cuba.
Obama asifu makubaliano ya kihistoria
Amepongeza kufikiwa kwa makubaliano ya kihistoria kama makubaliano ya mazingira ya Paris yanayolenga kupunguza joto duniani, makubaliano kati ya Iran na nchi zenye nguvu zaidi duniani kuhusu mpango wake wa kinyuklia na ufanisi katika kukabiliana na virusi vya Ebola katika nchi za magharibi mwa Afrika.
Masuala mengine ambayo ameyaangazia katika hotuba yake ya mwisho ni kufungwa kwa gereza la Guantanamo ambapo amesema atajaribu kulifunga, kushughulikia mizozo duniani hasa katika kanda ya mashariki ya kati, mabadiliko ya hali ya hewa, nishati na vita dhidi ya Malaria.
Rais huyo amekiri kuwa wakati wa utawala wake mvutano baina ya vyama vikuu nchini Marekani ulishamiri badala ya kupungua, akisema hali hiyo ni mojawapo ya masuala machache anayojutia katika kipindi chake kama Rais.
Mwandishi: Caro Robi/afp/reuters/dpa
Mhariri: Gakuba Daniel