1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama atoa hotuba ya mwisho kuhusu usalama

7 Desemba 2016

Rais wa Marekani, Barack Obama ametoa hotuba yake ya mwisho kuhusu usalama wa taifa, kabla hajakabidhi madaraka kwa Rais ajaye, Donald Trump. Obama amesema mapambano dhidi ya ugaidi hayapaswi kukanyaga haki za kiraia. 

USA Präsident Obama besucht MacDill Air Force Base
Picha: Reuters/K. Lamarque

Akizungumza katika hotuba hiyo aliyoitoa jana kwenye kambi ya jeshi la Anga ya MacDill, Tampa, Florida, Rais Obama ametetea rekodi yake katika kupambana na ugaidi na kuzuia suala la kupeleka wanajeshi wengi, na kuongeza kuwa vita dhidi ya ugaidi haipaswi kukandamiza haki za binadamu pamoja na misingi ya demokrasia ya Marekani.

''Tunahitaji hekima ya kuhakikisha tunashikilia maadili yetu na suala la kuheshimu utawala wa sheria sio udhaifu, bali linaonyesha nguvu yetu kubwa. Hivyo badala ya kutoa ahadi za uwongo kwamba tunaweza tukaondoa ugaidi kwa kudondosha mabomu au kupeleka majeshi zaidi au kujiwekea ukuta na kujitenga na maeneo mengine duniani, tunatakiwa kuwa na mtazamo wa muda mrefu kuhusu kitisho cha ugaidi na tunapaswa kuwa na mkakati madhubuti ambao utakuwa endelevu,'' amesema Obama.

Mara baada ya kuingia madarakani, Rais Obama alipiga marufuku mbinu zilizokuwa zinatumiwa na Shirika la Ujasusi la Marekani-CIA, kuwahoji washukiwa wa ugaidi. Ameupongeza uamuzi wake wa kupiga marufuku utesaji kwenye maeneo yote katika kipindi chote, kama vile mbinu ya kumziba uso kwa kitambaa mtuhumiwa, kumfunga katika ubao na kisha kumwagia maji mwilini.

Obama asikitishwa kutotimiza ahadi ya kuifunga Guantanamo Bay

Hata hivyo, Rais Obama ameelezea masikitiko yake kutokana na kushindwa kulifunga gereza la Guantanamo Bay, kama alivyoahidi. Amesema Marekani ilikuwa inapoteza mamia ya mamilioni ya Dola kwa kuwahudumia chini ya wafungwa 60 wanaoshikiliwa katika gereza hilo lililoko Cuba.

Rais Barack Obama akihutubia katika kambi ya jeshi la anga MacDillPicha: Reuters/K. Lamarque

Akizungumza huku akipigiwa makofi, Rais Obama pia amesisitiza kwamba Marekani inapaswa kulinda haki za Waislamu na kuwashtaki watuhumiwa wa ugaidi katika mahakama za kiraia. Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump alielezea kuunga mkono utesaji na pia ametaka Waislamu wapigwe marufuku kuingia Marekani. Obama amesema wanaweza kuwapata magaidi, lakini amekiri kuwa msimamo mkali utaendelea kuwepo kwa miaka mingi inayokuja.

Kiongozi huyo amefafanua kwamba majeshi ya Marekani yameondolewa Iraq na Afghanistan tangu alipochukua madaraka mwaka 2009 kutoka kwa mtangulizi wake, George W. Bush. Chini ya utawala wa Obama, idadi ya wanajeshi kwenye nchi hizo mbili imepungua kutoka 180,000 hadi 15,000. Idadi hiyo inajuwamuisha washauri waliokuwepo nchini Syria.

Amesema mkakati huo umefanikiwa kuwarudisha nyuma wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu-IS, ambalo amesema limepoteza udhibiti mkubwa wa maeneo yenye wakaazi wengi.

Aidha, Rais Obama amesema Marekani ni taifa linaloamini kwamba uhuru wa mtu hauwezi kuchukuliwa kwa mzaha na kwamba kila mmoja ana wajibu wa kuzingatia hilo. Raia wana haki ya msingi ya kutoa mawazo, kuishi kwenye jamii iliyo huru na yenye uwazi, ambayo inaweza kumkosoa hata rais bila ya kuadhibiwa, amesisitiza rais huyo.     

 

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, DPA, AP
Mhariri: Daniel Gakuba

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW