Obama atua Indonesia
9 Novemba 2010Baada ya kuahirisha safari yake mara mbili, hatimaye leo hii (9 Novemba 2010), Rais Barack Obama anawasili Indonesia, nchi ambayo iliwahi kumlea utotoni mwake. Waindonesia walikuwa wanaisubiria ziara hii kwa hamu si kwa kuwa tu wana historia binafsi na Rais Obama, bali kutokana na matarajio kwamba kiongozi huyu anaweza kubadilisha siasa za msuguano kati ya Marekani na ulimwengu wa Kiislamu, kwani Indonesia ni taifa lenye Waislamu wengi zaidi duniani.
Kama ilivyokuwa kwa India, ambako amemaliza ziara yake ya siku nne, nchi hizi Marekani na Indonesia nazo zina mengi ya pamoja. Lakini, suala la haki za binaadamu linaonekana kuwa kikwazo katika mazungumzo ya leo (9 Novemba 2010) kati ya Rais Obama na mwenzake Susilo Bambang Yudhoyono.
Rikodi za vikosi vya kijeshi vya Indonesia, hasa kile cha Kopassus, zinaonesha uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu katika maeneo ya Timor ya Mashariki, Papua ya Magharibi na Acheh.
Mataifa haya mawili yana uhusiano wa muda mrefu chini ya kile kinachoitwa vita dhidi ya ugaidi. Kikosi maalum cha kupambana na ugaidi cha Indonesia kiitwacho Detachment 88, na ambacho kilianzishwa mwaka 2002 baada ya mashambulizi ya Bali, kinafadhliwa kwa hali na mali na Marekani na Australia, na kimekuwa na mafanikio makubwa. Hivi sasa makundi yanayojinasibisha na Al Qaeda yamesambaratishwa na viongozi wake wengi wameuawa au kushikiliwa na Detachment 88.
Jambo jengine linazozikutanisha nchi hizi mbili ni hofu za kila mmoja wao kwa China. Kwa Marekani, China ni taifa linalokuja juu kwa kasi kuipiku hasa katika uzalishaji wa bidhaa na nguvu ya fedha, na kwa Indonesia, China ni taifa linalotanua misuli yake kwa nguvu katika eneo zima la Kusini mwa Asia, jambo ambalo linatishia uchumi na siasa za eneo hilo.
Ndio maana si ajabu, kama anavyosema makamo wa rais wa taasisi ya Serukindo Global Consulting ya nchini Indonesia, Noor Huda Ismail, kwa Rais wa Marekani kuichukulia Indonesia kama rafiki mwema, hata kama Indonesia ina matatizo yake ya uvunjaji wa haki za binaadamu katika siasa za ndani.
Kwa hivyo, Obama analazimika kutumia siasa za "nikune-mgongoni-mwangu-nikukune-na-wako" atakapokutana na mwenzake Yudhoyono, ili kila mmoja apate muradi wake kwa mwenziwe. Marekani iendeleze urafiki na moja ya mataifa makubwa kwenye Asia ya Kusini ili kupunguza nguvu za adui anayeinukia wa China na Indonesia iendelee kupata misaada ya kifedha na kiusalama kutoka kwa taifa lenye nguvu kubwa ya kijeshi la Marekani bila ya kuonesha wazi upinzani wake kwa China.
Hata hivyo, siasa za Marekani kuelekea Indonesia zinakosolewa sana. Kwa mfano, wakati Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Robert Gates, alipotangaza mwezi Julai mwaka huu kwamba nchi yake inaondoa vikwazo vya kutoshirikiana na Kopassus kutokana na kundi hilo kuwaondoa watuhumiwa wote wa uvunjaji wa haki za binaadamu, wanaharakati walikosoa kwamba bado Kopassus inaendelea na mateso yake kama kawaida, wakitolea mfano picha ya video iliyooneshwa hivi karibuni ambapo kikosi hicho kinafanyia mahojiano wenyeji wa Papua ya Magharibi kwa kuwapiga na kuwatesa.
Kwa upande mwengine, Waislam nchini humo wanasema kwamba Marekani inajali zaidi suala la haki za binaadamu inapokuwa linahusiana na Wakristo tu na si kinyume chake. Timor ya Mashariki na Papua ya Magharibi ni sehemu zenye Wakristo wengi, na ambazo mara kadhaa Marekani imepaza sauti yake kukemea uvunjaji wa haki za binaadamu, lakini si kwa Acheh ambayo ina Waislam wengi.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Josephat Charo