1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama atunukiwa zawadi ya amani ya Nobel

Oumilkher Hamidou9 Oktoba 2009

Walimwengu waelezea matumaini yao kuona amani inaimarishwa ulimwenguni

Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: AP

Hongera zinazidi kumiminika baada ya tuzo ya amani ya Nobel kutunukiwa bila ya kutegemewa rais wa Marekani Barack Obama.Lakini pia miito ya kushadidia juhudi za amani ulimwenguni imehanikiza.

"Tuzo hii ya amani inawapa moyo wote wale wanaopendelea kua na ulimwengu ulio salama zaidi" amesema mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso,huku kansela wa Ujerumani akiutaja uamuzi wa kamati ya Nobel kua ni "kichocheo" cha kuzidisha juhudi za amani.

"Kwa muda mfupi tuu,Obama amefanikiwa kuanzisha utaratibu mpya na kufungua njia ya mazungumzo,amesema kansela Angela Merkel pembezoni mwa sherehe za kuadhimisha miaka 20 ya "mapinduzi ya amani" ya Leipzig,yaliyopelekea kuporomoka ukuta wa Berlin,November 9 mwaka 1989.

Kansela Angela Merkel amesisitiza

"Nnamini sote tunabidi tumuunge mkono,ili amani iweze kupatikana haraka ulimwenguni."

Shirikisho la kimataifa la jumuia za haki za binaadam linaamtaka mshindi wa mwaka huu wa zawadi ya amani ya Nobel,atekeleze kivitendo juhudi zake.

Barack Obama,rais wa kwanza mwenye asili ya kiafrika,kuwahi kuiongoza Marekani,ametunukiwa zawadi ya amani ya Nobel kwa "kuanzisha enzi mpya katika siasa za kimataifa"-kwa mujibu wa kamati ya Nobel.

Iran ambayo uhusiano wake na Marekani ni tete,ilikua miongoni mwa nchi za mwanzo kutoa kutamka inategemea zaqwadi ya amani ya Nobel itamsaidia rais wa marekani katika kuimarisha juhudi zake za amani.

Kamati ya Nobel imepitisha uamuzi huo katika wakati ambapo rais wa Marekani anakabiliwa na mivutano miwili;wa kwanza nchini Irak na wa pili nchini Afghanistan.

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan amesema anaamini rais Obama anastahiki kutunzwa zawadi ya amani katika wakati huu ambao anatafakari juu ya uwezekano wa kutumwa au la wanajeshi zaidi kukabiliana na wataliban.

Lakini wataliban wameukosoa uamuzi wa kamati ya Nobel wakisema "hawaoni mabadiliko yoyote ya kimkakati kuelekea amani."

Obama ameleta matumaini ya amani ulimwenguni" amesema kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa la nguvu za atomiki Mohammed el Bbaradei.

Kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas ameelezea matumaini yake kuona amani ikienea Palastina na Mashariki ya kati kwa jumla chini ya uongozi wa Barack Obama.

Rais wa zamani wa Poland,Lech Walesa ameduwaa alipopata habari za kutunukiwa Barack Obama zawadi ya amani ya Nobel.Kiongozi huyo wa zamani wa chama cha wafanyakazi wa Poland amesema tunanukuu:"Nani,Obama.Mbona haraka.Hajapata wakati wa kufanya chochote.Kwasasa anapendekeza tuu."Mwisho wa kumnukuu.

Nchini Ufaransa rais Nicolas Sarkozy amempongeza rais Obama na kusifu juhudi zake katika kutanguliza mbele diplomasia na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.Tuzo hiyo ni ushahidi kwamba Marekani imerejea sasa katika nyoyo za walimwenguni." Amesema rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy.

Rais wa Urusi Dimitri MedvedevPicha: picture-alliance/ dpa

Na rais wa Urusi Dimitri Medvedev ameleezea matumaini ya kuziona Washington na Moscow zikifikia makubaliano ya kupunguza silaha,muda wa makubaliano ya sasa ya START-utakaapomalizika mwishoni mwa mwaka huu.

Mwandishi: O.Hamidou/rtr/afp

Mhariri:Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW