1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama aunyoshea mkono ulimwengu wa kiislamu

7 Aprili 2009

Rais Obama amekutana na viongozi wa dini mbali mbali huko Istanbul,Uturuki leo.

Rais Barack Obama na Rais Abdullah Gul wa utruki)Picha: AP

Akikamilisha ziara yake iliomchukua kwanza katika mkutano wa kilele wa mataifa 20 tajiri mjini London,Strassbourg,Ufaransa kwa sherehe za miaka 60 za shirika la NATO,Prague ,Jamhuri ya Czech alikochambua ndoto yake ya ulimwengu bila ya silaha za kinuklia,Rais Barack Obama wa Marekani amekutana leo na viongozi wa dini na mbali mbali mjini Istanbul,Uturuki kabla hakuondoka adhuhuri hii kurejea Marekani.

Katika ajenda yake ya leo alizuru msikiti maarufu wa "Blue Mosque", Kanisa mashuhuri la zamani lililogeuka makumbusho la "Divine Wisdom"-alama maarufu za jiji la Istanbul na mwishoe, akazungumza na wanafunzi katika juhudi zake za kukinyoshea mkono wa suluhu kizazi cha siku zijazo cha waiislamu ulimwenguni.

Rais Barack Hussein Obama, alikwishauambia ulimwengu wa kiislamu jana akihutubia Bunge la Uturuki, kuwa nchi yake ya Marekani haiupigi vita uislamu.Akijaribu hapo kufuta doa katika heba ya Marekani sio tu ulaya bali hata katika ulimwengu wa kiislamu kwa jumla.Barack Hussein Obama, amekutana leo na wajumbe wa dini ya kiislamu,kiyahudi na wa makanisa ya madhehebu tofauti ya kikristu katika hoteli yake mjini Istanbul.Baadae, alianza ziara ya kutembelea vituo vya kihistoria vya jiji hilo la Uturuki.

"Niruhusuni niseme tena kwa uwazi kabisa kama niwezavyo: Marekani ,haiko na haitakua vitani na uislamu." aliliambia Bunge la Uturuki,nchi ya kwanza kubwa ya kiislamu anayotembelea Obama tangu kushika hatamu mjini Washington.Isitoshe, alionya kwa kusema huwezi kuzima moto kwa kuchochea moto, akiwasia kwamba nguvu pekee haziwezi kukandamiza siasa kali .Akaongeza kusema ,

"Tutasikiliza kwa makini,tutasuluhisha tofauti.... tutaonesha heshima hata ikiwa hatukubaliani."Alisema Obama akiahidi kutangaza miradi maalumu ya kibiashara,elimu na afya katika ulimwengu wa nchi za kiislamu.alisema zaidi : '"

Marekani imeneemeshwa na wamarekani wa dini ya kiislamu.Wamarekani wengi wengineo wana jamaa zao wa kiislamu katika ukoo wao au wameishi katika nchi za kiislamu.Najua hayo kwa sababu binafsi ni mmojawao."

Rais Obama akaionyoshea tena mkono wa suluhu Iran,aliungamkono mazungumzo baina ya Israel na Syria na akaahidi kufanya juhudi mpya baada ya kupita miezi kadhaa tu kuboresha huduma za afya ,elimu na biashara na ulimwengu wa kiislamu.

Katika medani ya kisiasa,Rais Obama alikariri kuungamkono kwa nchi yake ya Marekani hodi hodi inazopiga Uturuki kujiunga na umoja wa Ulaya.Aliunga tena mkono suluhisho la dola mbili -ile ya Israel na ya wapalestina katika mgogoro wa mashariki ya kati. Akakumbusha rais Obama:

"Hiyo ndio shabaha ilioafikiwa na pande zote katika mpango wa "roadmap" na katika maafikiano ya Annapolis. Na hii ndio shabaha nitakayoifuata kwa juhudi kubwa nikiwa rais."

Kuhusu mkono alioinyoshea Jamhuri ya kiislamu ya Iran, rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran ,aliupokea mkono huo hapo jana lakini alisema Iran inasubiri hatua madhubuti za kivitendo kufuata maneno. Rais Obama amemaliza ziara yake hivi punde nchini Utruuki, baada ya kuzungumza na wanafunzi wa Uturuki na kuwapa salamu za kutoa kwa kizazi kijacho cha waislamu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW