1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama awahimiza vijana kuendeleza mapambano ya mazingira

Sylvia Mwehozi
9 Novemba 2021

Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama amewatolea wito wanaharakati vijana wa mazingira kuendeleza mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia. 

Barack Obama I UN-Klimakonferenz COP26 in Glasgow
Picha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama amekutana na viongozi wa vijana katika mkutano wa kimataifa wa mazingira unaoendelea mjini Glasgow COP26, kwa ajili ya kujadili jinsi gani ya kupiga hatua katika ahadi zilizotolewa mwaka 2015 katika mkataba wa Paris. Obama amezikosoa China na Urusi kwa "kukosa udharura" katika kupunguza gesi chafu.Ulimwengu waadhimisha miaka mitano ya mkataba wa Paris

"Hata kama nchi tajiri, nchi zilizoendelea zote zitafanya inavyopaswa kufanyika, ikiwa India na China zinakwenda sambamba na sisi, haijalishi tunafanya nini. Bado tutakuwa chini ya futi nne za maji, sawa?"

Rais huyo wa zamani wa Marekani ni miongoni mwa viongozi wa ulimwengu waliohusika katika mkataba wa Paris wa mwaka 2015. Kiongozi huyo amefika katika mkutano wa COP26 mjini Glasgow na kuwahimiza wanaharakati vijana wa mazingira kuendeleza mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.

Baadhi ya wanaharakati vijana kama Ross Hamilton mwenye umri wa miaka 19 wanaonekana kuwa na matumaini na Obama kama kiongozi mwenye kusema ukweli. Hata baada ya miaka mitano ya kumaliza uongozi wake, Obama ambaye sasa ana umri wa miaka 60 ameendelea kuwa maarufu miongoni mwa vijana katika namna ambayo rais Joe Biden hawezi kufikia.

Picha: Getty Images/AFP/P.P. Marcou

Wakati akiwa rais, Obama alianzisha mipango ya kuielekeza zaidi Marekani kuelekea nishati mbadala na kuachana na makaa ya mawe, ingawa rais Donald Trump aliondoa mipango karibu yote.

Hata hivyo si wanaharakati wote vijana ambao ni shabiki wa Obama. Mwanaharakati kijana wa Uganda Vanessa Nakate aliandika kupitia Twitter kwamba alikuwa na umri wa miaka 13 wakati Marekani chini ya utawala wa Obama ilipokuwa miongoni mwa mataifa tajiri kuahidi dola bilioni 100 kwa mwaka. Pesa hizo zililenga kuyasaidia mataifa maskini katika mapambano na kukabiliana na ongezeko la joto, lakini anadai kwamba mataifa hayo tajiri yamevunja ahadi zake.

Wanaharakati vijana hususan barani ulaya, wamekuwa na shinikizo dhidi ya serikali katika kushughulikia suala la mabadiliko ya tabia nchi. Miongoni mwao ni mwanaharakati kinara Greta Thunberg ambaye mwaka 2018 alianzisha harakati za mazingira ambazo tangu wakati huo zimevutia maelfu ya vijana kufanya maandamano ya kila wiki ya kuzitaka serikali kuacha utegemezi katika makaa ya mawe, gesi asilia na mafuta.

Obama anasema kumekuwa na maendeleo kiduchu tangu makubaliano ya Paris ya 2015 ya kupunguza joto kufikia nyuzi joto 1.5.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW