Obama awaonya wagombea Afghanistan
9 Julai 2014Rais Barrack Obama pia ametishia kusimamisha msaada wa Marekani kwa Aghanistan, Iwapo mmoja ya wagombea atachukua madaraka kinyume cha sheria au iwapo kutachukuliwa hatua zilizoko nje ya katiba.
Rais Barrack Obama alimpigia simu kiongozi anayeongoza kwa wingi wa kura nchini Aghanistan Ashraf Ghani Ahmadzai siku moja baada ya kuzungumza na mpizani wa Ghani, Abdulla Abdulla.
Kulingana na Ikulu ya Marekani, Obama aliwaambia wagombea wote wawili, kwamba Marekani inatarajia madai yote ya udanganyifu wa kura yatachunguzwa kwa uadilifu mkubwa, huku akiwatolea mwito wagombea hao wawili kuchukua hatua ambazo hazitaihatarisha Umoja wa Kitaifa.
Aidha msemaji wa ikulu hiyo Josh Earnest amesema Rais Obama alikuwa wazi kabisa juu ya msimamo wa Marekani kwa kile kinachoendelea nchini Afghanistan.
"Rais aliweka wazi kama tunavyosema hadharani ni kwamba, tunatarajia tathmini ya kina ya madai yote ya udanganyifu, na kwamba na kwamba hakuna maana kwa kufikia uamuzi wa kuanzisha vurugu au kuchukua hatua zilizoko nje ya katika,”alisema Josh Earnest.
Onyo hilo linaonekana kumlenga moja kwa moja Abdulla Abdulla, aliyewaambia maelfu ya wafuasi wake hapo jana kuwa yeye ndiye mshindi wa uchaguzi wa mwezi uliopita , huku kukiwa na miito ya kuunda serikali sambasamba kutoka kwa wafuasi hao.
Tume ya uchaguzi bado haijamtangaza mshindi
Siku ya Jumatatu tume huru ya uchaguzi nchini Afghanistan ilitoa matokeo ya mwanzo ya uchaguzi yaliomuonesha Ashraf Ghani akiongoza kwa asilimia 56 ya kura huku Abdulla Abdulla akijipatia asilimia 44 ya kura.
Tume hiyo imesema hakuna mshindi aliyetangazwa rasmi kutokana na uchunguzi unaoendelea juu ya madai ya wizi wa kura. Abdullah ndiye aliyeongoza katika duru ya kwanza lakini akakosa idadi inayohitajika kuwa mshindi wa moja kwa moja.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Anders Fogh Rasmussen amesema madai yaliotolewa yanatia wasiwasi. Amewahimiza viongozi wote wawili kufanya kazi kwa karibu na tume ya uchaguzi kutafuta suluhu ya kuhakikisha kunakuwepo na matokeo ya kuaminika .
Haya yote yanatokea wakati Marekani ikiwa katika harakati za mwisho za kuwaondoa wanajeshi wake takriban 50,000 nchini Afghanistan baadaye mwaka huu baada ya kumaliza jukumu lao la kupambana na waasi wa Taliban.
Hata hivyo wataalamu wanasema misimamo inayoonekana kwa sasa kati ya wagombea hao wawili wa Urais nchini Afghanistan, imeongeza wasiwasi wa kutokea ghasia za kikabila na kurejea tena kwa mgogoro kati ya wababe wa kivita walioisambaratisha Afghanistan kuanzia mwaka wa 1992 hadi mwaka 1996 katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mwandishi: Amina Abubakar/AP/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman