Obama awasifu washirika wa Kiarabu dhidi ya IS
23 Septemba 2014Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu majeshi ya nchi yake kulishambulia kundi la IS, ndani ya ardhi ya Syria, Rais Obama amesifu mchango wa mataifa ya Kiarabu yaliyoungana na Marekani kwenye mashambulizi hayo, akizitaja hasa nchi Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Jordan, Bahrain na Qatar, hatua aliyosema inaashiria Marekani inaungwa mkono na dunia.
Katika hotuba hiyo aliyoitoa muda mfupi kabla ya kuelekea kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa anakotarajiwa kuzidi kusaka uungwaji wa kampeni yake dhidi ya IS, Obama amesisitiza umuhimu wa umoja wa pande hasimu za kisiasa ndani ya Marekani katika kuling'oa kabisa kundi hilo, ingawa amekiri kuwa si kazi itakayochukuwa muda mfupi
"Kampeni hii itachukua muda. Kutakuwa na changamoto huko twendako. Ila tutafanya kila tuwezalo kulikabili kundi hili la kigaidi kwa usalama wa nchi, eneo hilo waliko na dunia nzima."
Rais Obama anatazamiwa kuongoza kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzungumzia wapiganaji wa kigeni wa IS walio na paspoti za kusafiria za mataifa ya Magharibi.
Ikiungwa mkono na mataifa hayo, usiku wa kuamkia leo Marekani ilivishambulia vituo kadhaa vya IS pamoja na kundi liitwalo Khorasan, linaloundwa na wapiganaji wa al-Qaida na Obama amesema lilikuwa linapanga mashambulizi dhidi ya majeshi ya nchi za Magharibi.
Mataifa ya GCC yashiriki kikamilifu
Nchini Bahrain, shirika la habari la BNA limelinukuu jeshi likisema kwamba nchi hiyo pamoja na wanachama wengine wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba, GCC, walituma ndege kwenye mashambulizi hayo liliyosema ni dhidi ya "maeneo ya kigaidi". Kauli hiyo ni ya kwanza kutolewa na taifa hilo la Ghuba tangu kufanyika kwa masambulizi.
Taarifa zinasema kiasi cha wapiganaji 115 wa IS wameuawa kwenye mashambulizi hayo yaliyofanyika kwenye vituo zaidi ya 20, huku msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani, Admirali John Kirby, akisema bado wanatathmini ufanisi wa mashambulizi hayo.
Balozi wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa, Bashar Ja'afari, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba alifahamishwa juu ya mashambulizi hayo na mwenzake wa Marekani, Samantha Power.
Nayo Uingereza imetangaza kuwa tayari kujiunga rasmi na Marekani kwenye mashambulizi ya anga dhidi ya wanamgambo wa IS. Waziri Mkuu David Cameron amesema hivi leo kwamba atasaka ridhaa ya bunge kuchukua hatua hiyo.
Hapo kesho, Waziri Mkuu huyo atazungumza kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo anatazamiwa kutoa wito wa dunia kuungana kuliangamiza kundi la IS, ambalo ameonya kwamba linapanga kuishambulia Uingereza.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP/dpa
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman