Obama awasili barani Ulaya
23 Mei 2011Rais Barack Obama amewasili rasmi Ulaya, akianza ziara ya siku tatu. Amewasili asubuhi ya leo mjini Dublin, nchini Ireland. Katika ziara hiyo pamoja na kutembelea Ireland ambako atakwenda katika kijiji kidogo ambacho wanatokea mababu zake wa upande wa mama yake, pia atahudhuria mkutano wa kundi la mataifa yenye utajiri wa viwanda G8 utakaofanyika nchini Ufaransa. Mada kuu zitakazojadiliwa ni pamoja na suala la uchumi duniani pamoja na hali katika mataifa ya Kiarabu.
Rais Barack Obama atakuwa nchini Ireland kwa muda wa saa 24 ambako atatembelea kijiji ambacho wanatokea mababu zake wa upande wa mama yake. Katika kijiji hicho cha Moneygall bado wanaishi binamu zake wa mbali. Mmoja wa mabinamu hao ni Henry Healy.
"Hatujawahi kuwa karibu na rais. Lakini sasa imekuwa kweli. Anakuja katika kijiji cha Moneygall, mahali ninapoishi."
Mababu kutoka ukoo wa mama yake wametokea katika kijiji cha Moneygall ambapo walihamia Marekani katika mwaka 1850. Watu wachache, hata hivyo, wataruhusiwa kumlaki Obama wakati akiwa katika kijiji hicho. Amepangiwa kuonana na mabinamu zake 16 tu.
Baada ya ziara yake nchini Ireland Obama anatarajiwa kuzuru Uingereza na Poland katika hatua ya kuuendeleza uhusiano kati ya Marekani na nchi hizo.Wakati wa ziara yake ya kwanza barani Ulaya, kulidhihirika hali ya hamasa katika mwazo mpya wa uhusiano baina ya Marekani na mataifa ya Ulaya, lakini mara hii uhusiano baina ya pande hizo mbili uko bado katika hali ya mivutano.
Wakati huo huo, rais Barack Obama jana Jumapili ameendelea kutetea mtazamo wake kuhusiana na makubaliano ya amani ya mashariki ya kati kufuatia hatua ya waziri mkuu wa Israel ya kumshambulia hadharani. Obama alitoa ujumbe wake mbele ya waungaji mkono wakubwa wa Israel, akionya kuwa kundi linalounga mkono Israel la mjini Washington kuwa matokeo ya kuendelea kuwa na mkwamo katika hatua za kuleta amani katika mashariki ya kati kunaweza kuleta madhara kwa taifa hilo la Kiyahudi.
Mzizi wa fitina hapa ni kuhusu wito wa Obama kuwa mipaka iliyokuwapo mwaka 1967 kabla ya vita kati ya mataifa ya Kiarabu na Israel kuwa ndio msingi wa taifa la Palestina.
Waziri mkuu wa Israel alilikataa kabisa wazo hilo, akitafsiri wito huo kuwa ni wa kurejea katika mipaka kamili, na kusema kuwa kijeshi mipaka hiyo ya zamani haiwezi kulindwa.
Lakini jana jumapili Obama amewaambia wajumbe katika tume ya kushawishi maslahi ya Israel katika Marekani kuwa dai hilo linakwenda kinyume na wito wake huo na kupuuzia wito wake wa makubaliano ya pamoja na mabadiliko ya mipaka. Obama alisema .
"Kwa sababu tunafahamu changamoto zinazoikabili Israel, mimi pamoja na utawala wangu tumelifanya suala la usalama wa israel kuwa muhimu. Ndio sababu tumeongeza ushirikiano baina ya majeshi yetu katika kuwango cha juu kabisa."
Baada ya kuukataa mpango wa rais Obama, hata hivyo waziri mkuu wa Israel leo anatarajiwa kutoa msimamo wake juu ya mtazamo wa Obama kuhusu vipi hatua za amani za mashariki ya kati zinaweza kutekelezwa, wakati atakapohutubia kundi linaloangalia maslahi ya Israel nchini Marekani.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe/rtre
Mhariri : Othman Miraji