1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama azungumta tena na Putin kuhusu Ukraine

15 Aprili 2014

Rais Barack Obama wa Marekani amemtaka Rais Vladimir Putin wa Urusi kuyashinikiza makundi yenye kuiunga mkono Urusi yalioko Ukraine kusalimisha silaha zao wakati mzozo huo ukizidi kupamba moto. .

Vikosi vya Ukraine vikiwa nje ya mji wa Slavjansk. (14.04.2014)
Vikosi vya Ukraine vikiwa nje ya mji wa Slavyansk. (14.04.2014)Picha: picture-alliance/ITAR-TASS

Taarifa ya Ikulu ya Marekani imesema kwamba Obama alitowa wito huo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Rais Putin kufuatia ombi la Urusi la kutaka kuwepo mazungumzo hayo na kwamba Obama ameituhumu serikali ya Urusi kwa kuunga mkono wanaharakati wanaotaka kujitenga wanaoiunga mkono Urusi ambao wanakusudia kuidhoofisha na kuiyumbisha serikali ya Ukraine .

Obama amemwambia Rais Putin kwamba vikosi visio rasmi nchini humo inabidi viweke chini silaha zao.

Putin amekanusha kuhusika katika uasi wa wanaharakati wanaoiunga mkono Urusi lakini Umoja wa Ulaya ambayo haisadiki kauli hiyo ya Urusi imetanuwa wigo wa vikwazo vyake kwa maafisa wanaotuhumiwa kutaka kuligawa jimbo hilo la zamani la muungano wa Kisovieti.

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya waliokuwa wakikutana Luxembourg wametangaza kwamba wanatanuwa orodha ya maafisa 33 wa Urusi na Ukraine na viongozi wa biashara waliowekewa vikwazo vya kuzuiliwa kwa mali zao na marufuku ya viza kutokana na dhima yao katika mzozo huo wa Ukraine.

Urusi yakanusha kudhamini uasi

Kwa mujibu wa maelezo ya serikali ya Urusi kuhusu mazungumzo baina ya Obama na Putin, kiongozi huyo wa Urusi amemwambia Obama kwamba Urusi haiwadhamini wanaharakati hao wanaotaka kujitenga wenye bunduki za Kalashnikov mkononi ambao wamenyakuwa majengo kadhaa muhimu ya serikali mashariki mwa Ukraine.

Rais Vladimir Putin wa Urusi.Picha: Reuters/Mikhail Klimetyev/RIA Novosti

Putin amemuhimiza Obama kufanya kila linalowezekana kuepeusha matumizi ya nguvu na umwagaji damu.

Rais Oleksandr Turchynov wa Ukraine anayeungwa mkono na mataifa ya magharibi amekuwa akitafuta njia ya kuondokana na mzozo huo unaozidi kupamba moto kwa kupendekeza kura ya maoni juu ya kupewa mamlaka makubwa zaidi kwa majimbo ya nchi hiyo na kutaka msaada kutoka Umoja wa Mataifa.

Tutchynov pia amemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kusaidia katika kufanya operesheni ya pamoja dhidi ya ugaidi mashariki ya Ukraine.Bado hakuna jibu kutoka Umoja wa Mataifa na ofisi ya rais huyo wa Ukraine haikufafanuwa ni msaada wa aina gani hasa inaouomba nchi hiyo.

Operesheni dhidi ya ugaidi

Hapo Jumapili serikali ya Ukraine iliahidi kufanya operesheni kamili ya kupambana na kile ilichokiita ugaidi dhidi ya wanaharakati wanaotaka kujitenga lakini hadi sasa operesheni hiyo imeshindwa kutekelezwa.

Rais wa mpito wa Ukraine Alexander Turchynov.Picha: picture-alliance/Itar-Tass/Maxim Nikitin

Kwa upande mwengine waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov leo amekaribisha dalili kwamba serikali ya Ukraine iko tayari kwa mazungumzo na wanaharakati wanaotaka kujitenga mashariki ya Ukraine na kuziita dalili hizo kuwa ni hatua kwenye mwelekeo sahihi.

Akizungumza akiwa ziarani mjini Beijing China amesema kule kunakoonekana kuwa tayari kwa serikali ya Ukraine kuyapatia ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo matatizo yote kuhusiana na madai halali ya wakaazi wake wa majimbo kusini na mashariki ya Ukraine hakia niu hatua kwenye mkondo sahihi licha ya kwamba hatua hiyo imechelewa mno kuchukuliwa.

Mwandishi: Mohamed Dahman/ AFP/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu