Obama azungumza na Poroshenko
4 Juni 2014Wakati huo huo mataifa yenye utajiri mkubwa wa viwanda dunia yanakutana bila ya Urusi kwa mara ya kwanza katika miaka 17 mjini Brussels.
Mkutano kati ya rais wa Ukraine Petro Poroshenko na Barack Obama mjini Warsaw ulikuja siku kumi baada ya tajiri huyo mkubwa nchini Ukraine mwenye kiwanda cha kutengenezea chokoleti alipochaguliwa kuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo tangu rais aliyekuwa akipendelea Urusi kukimbia na Urusi kuiunganisha rasi ya Crimea katika mvutano ambao umezusha mtengano duniani.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry alikutana na Poroshenko kabla ya rais Obama kukutana nae katika hoteli ya Marriott mjini Warsaw, na kusema Marekani inatashiriki katika sherehe za kuapishwa kwa Poroshenko hapo siku ya Jumamosi.
Obama amuonya Putin
Obama alikuwa mjini Warsaw katika kumbukumbu ya miaka 25 ya sehemu ya uchaguzi wa kwanza huru wa Poland, ikiwa ni mfano wa hatua za kidemokrasia ambapo rais wa Marekani anapanga kuizungumzia katika hotuba yake leo Jumatano kuwa ni mfano kwa Ukraine.
Obama amemuonya rais wa Urusi Vladimir Putin kutokuendelea kuleta mgawanyiko nchini Ukraine na badala yake atambue ushindi wa rais Poroshenko na kuanza kujenga hali ya kuaminiana na mataifa ya magharibi.
"Usalama wa mashirika wetu katika eneo la Ulaya ya kati na mashariki ni muhimu sana kwa usalama wetu na ni wa kulindwa kwa gharama yoyote ile."
Viongozi wa dunia bila ya Vladimir Putin katika kundi la mataifa saba yenye utajiri mkubwa wa viwanda duniani wanaanza mkutano wao mjini Brussels ambao hapo kabla ulipangwa kufanyika ukimjumuisha rais Putin katika mji wa kitalii wa Sochi nchini Urusi .
Lakini katika siku za hivi karibuni , viongozi wa Uingereza , Ufaransa na Ujerumani walikuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na kiongozi huyo wa Urusi , wakionesha mgawanyiko miongoni mwa mataifa ya magharibi ambayo yaliungana kuitenga Urusi kuhusiana na hatua zake za matumizi ya nguvu dhidi ya Ukraine.
Mkutano huo wa siku mbili utazungumzia masuala ya sera za mambo ya kigeni , uchumi, biashara na usalama wa nishati.
Usalama wa nishati ni suala nyeti
Suala la usalama wa nishati ni nyeti kwa mataifa ya Ulaya baada ya miezi kadha ya mvutano na Urusi , ambayo inatoa karibu theluthi ya mahitaji ya bara la Ulaya ya mafuta na gesi.
Wakati itakuwa ni mara ya kwanza katika muda wa miaka 17 kwa Urusi kutohudhuria baada ya kujiunga na kundi hilo la mataifa mwaka 1997, Putin bado atakuwa na mazungumzo na kila mmoja wa viongozi wa kundi hilo peke yake akianza na kansela wa Ujerumani Angela Merkel, David Cameron wa Uingereza na rais wa ufaransa Francois Hollande wiki hii, pembezoni mwa kumbukumbu ya miaka 70 ya kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia.
Uamuzi wa kuiondoa Urusi katika kundi hiloulifanywa na wanachama wengine wa kundi hilo mwezi Machi baada ya Urusi kuliingiza katika himaya yake jimbo la Crimea.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / ape
Mhariri:Mohammed Abdul Rahman