Obama azungumza na Putin kuhusu Ukraine
29 Machi 2014Ikulu ya Marekani imesema Rais Putin amempigia simu Obama baada pendekezo lililowasilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov mapema wiki hii. Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jay Carney alisema "Rais Obama amependekeza kwamba Urusi iweke majibu madhubuti ya kimaandishi"
Viongozi hao wote wawili wamekubaliana kwamba Waziri Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov wakutane tena kujadili hatua nyingine kwa ajili ya kuzingatia pendekezo hilo la kidiplomasia kwa lengo la kumaliza kabisa mgogoro wa Crimea.
Urusi lazima iondoe wanajeshi wake
Hata hivyo hakukuwa na zaidi kuhusu jitihada hizo za kidiplomasia lakini taarifa ya Ikulu ya Marekani inasema Obama ameelezea dhamira yake ya kutafuta suluhu ya kidiplomasia. Aidha inaongeza kueleza kwamba "jambo hilo linawezekana tu pale ambapo Urusi itaondoa majeshi yake na kutochukua hatua nyingine yoyote ya kuingia katika mipaka ya Ukraine" imeeleza taarifa hiyo.
Baadae afisa tawala mwandamizi alidokeza kuwa mjadala wa awali wa kuangalia uwezekano wa kutafuta suluhisho uligusia masuala ya kupelekwa waangalizi wa kimataifa, kuondoshwa kwa majeshi ya Urusi na kufanyika kwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Urusi na Ukraine.
Dhana ya kurudisha mataifa ya kisovieti
Kitendo cha Urusi kulichukua eneo la Crimea kunatengeneza upya mipaka ya Ulaya na kufungua upya Vita Baridi kati ya Mashariki na Magharibi. Msuguano wa kidiplomasia umeulazimisha Umoja wa Kujihami NATO kutupia jicho kijeshi katika maeneo ya iliyokuwa mataifa ya Jumuiya ya zamani ya Kisovieti kwa lengo la kudhibiti hamasa ya taifa hilo ya kutaka kupanua mipaka yake.
Rais Putin kwa mara ya kwanza amekiri kuwa jeshi lake lilihusika moja kwa moja katika eneo la Crimea , hatua ya awali ambayo viongozi wenye mtazamo wa kimagharibi mjini Kiev, wanaohofia pengine ni mpango wa kumega sehemu kubwa zaidi ya Ukraine.
Urusi kutoendeleza harakati za kijeshi
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema Putin amemuhakikishia kwamba hana mpango wa kuendelea na operesheni zake za kijeshi katika kanda hiyo. Rais Obama alimwambia mtangazaji wa kituo cha televisheni cha CBS kwamba kuna ushahidi wa wazi majeshi ya Urusi yanajiimarisha katika mipaka ya Ukraine.
Mapema wiki hii afisa usalama wa juu kabisa nchini Ukraine alisema kumeonekana takribani wanajeshi 100,000 wa Urusi katika maeneo ya karibu na Ukraine, idadi ambayo haijathibitishwa wala kukanushwa na upande wa Urusi.
Mwandishi: Sudi Mnette AFP
Mhariri: Sekione Kitojo