1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama: Kenya iongeze mapambano dhidi ya al Shabaab

25 Julai 2015

Rais wa Marekani Barack Obama leo (25.07.2015) amefanya mashauri na mwenyeji wake Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi na kujadili maswala kadhaa yakiwemo usalama, uwekezaji na uongozi.

Barack Obama in Kenia mit Präsident Uhuru Kenyatta bei gemeinsamer Konferenz in Nairobi
Rais Obama (kulia) na rais KenyattaPicha: Reuters/J. Ernst

Rais wa Marekani Barack Obama ameitaka Kenya kuongeza jitihada za kulikabili kundi la wanamgambo wa al Shabaab kutoka Somalia. Obama amesema Marekani inahitaji kushirikiana kwa karibu zaidi na Kenya kuliangamiza kabisa kundi hilo, ikiwa ni pamoja na kubadilishana taarifa za kijasusi. Kiongozi huyo amesema mitandao ya kundi la al Shabaab imedhoofishwa katika Afrika Mashariki lakini kitisho bado kingalipo.

"Tumelipunguza eneo linalodhibitiwa na Al-Shabaab. Tumefaulu kupunguza udhibiti wao nchini Somalia na kuidhoofisha mitandao yao hapa Afrika Mashariki. Hiyo haina maana tatizo limetatuliwa," alisema Obama wakati wa mkutano wa waandishi wa habari na mwenyeji wake rais Uhuru Kenyatta. "Tunaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa uwezo wa makundi ya kigaidi, lakini bado yanaweza kusababisha maafa," akaongeza kusema Obama.

Rais Obama ameandaliwa gwaride la heshima katika Ikulu ya Rais kabla kufanya mashauri na mwenyeji wake Uhuru Kenyatta. "Tumekuwa na mazungumzo ya kufanya na Rais Barack Obama juu ya maswala muhimu yanayohusu Kenya na Marekani kama vile usalama na uhusiano wa kimaendeleo miongoni mwa maswala mengine," alisema Uhuru.

Mikataba yasainiwa

Mikataba kadhaa ya ushirikiano imetiwa saini ukiwamo ule wa ushirikiano katika swala la ugaidi. Rais Obama amesema, "Leo tumezungumzia suala la kuimarisha uhusiano wetu wa kiusalama kama sehemu yetu ya maongozi pia tumezungumzia mikakati ya kukabiliana na itikadi kali hapa nchini na dunia nzima kwa ujumla."

Marais hao wawili leo asubuhi walifungua kongamano la sita la ulimwengu kuhusu ujasiriamali katika ofisi za kabla Rais Obama kuzuru eneo la shambulizi la bomu la Agosti 7 mwaka 1998 na kuweka shada la maua kama ishara ya kuwakumbuka wahanga wa shambulizi hilo lililotekelezwa katika ubalozi wa Marekani wakati huo.

Rais Obama alipokutana na familia yakePicha: Reuters/J. Ernst

Kwenye kongamano hilo la ujasiriamali Rais Kenyatta amesema, "Nchi hii na bara hili hatuwezi kusema hatufanyi makosa lakini bila shaka tunaweza kudai kwamba tunasonga mbele. Cha msingi nikwamba tuko katika safari tunayowaalika mjiunge nasi. Tunaona nafasi nzuri inahitaji kuheshimu haki za binadamu."

Kongamano hilo la ujasiriamali linahudhuriwa na wajumbe wapatao 4,000 kutoka mataifa 120 ulimwenguni. "Changamoto ni nyingi. Ni vigumu kupata mikopo, ni vigumu kupata mafunzo na ujuzi wa kuendesha biashara na zaidi ya yote ni vigumu kwa wanawake na vijana ambao hawapati nafasi za juu za uwekezaji."

Viongozi hao wawili wamewahimiza vijana kuzingatia ufumbuzi unaolenga kutatua matatizo la bara lla Afrika.

Kutokana na makubaliano hayo ya kibiashara, mipango inafanywa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi Marekani.

Ziara ya Rais Barrack Obama nchini Kenya haikuwa tu ziara ya kikazi bali pia kukutana na familia yake kwani alipata fursa ya kujiunga na jamaa zake kutoka kijiji cha Kogelo kaunti ya Siaya kwa chakula cha jioni katika hoteli moja ya kifahari alipowasili jijini Nairobi hapo jana.

Rais Obama hapo kesho anatarajiwa kutoa hotuba ya hadhara katika uwanja wa michezo wa kimataifa wa Kasarani na kisha kuondoka nchini kwenda Addis Ababa Ethiopia kwa kongamano la viongozi wa Umoja wa Afrika.

Mwandishi: Alfred Kiti/DW Nairobi

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW