Obama kujadili masuala ya bara la Afrika
22 Septemba 2009Lakini mkutano wake mmoja wa faragha ni chakula cha mchana pamoja na viongozi wa serikali na nchi za Kiafrika zilizo kusini mwa Sahara. Wakati wa mkutano huo maalum, Obama atapata nafasi ya kuzungumza na viongozi wa nchi za Kiafrika juu ya masuala yalio na umuhimu kwa viongozi hao. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice ambae hapo zamani alikuwa makamu wa waziri wa mambo ya nje na akishughulikia masuala ya bara la Afrika amesema, miongoni mwa mada zitakazopewa kipaumbele wakati wa mkutano huo ni kuongezeka kwa idadi ya vijana na njia ya kuwapatia kazi wananchi wao na kuzalisha nafasi za ajira, kuendeleza biashara na uwekezaji, pamoja na njia ya kuwapatia chakula watu wasio na uwezo.
Lakini Padre Gabriel Odima, rais wa kituo kinachotetea amani na demokrasi barani Afrika-(Africa Centre for Peace and Democracy)chenye makao yake nchini Marekani anasema, Obama asiyape kipaumbele masuala ya kijamii na uchumi tu, bali azingatie pia mada zinazohusika na haki za binadamu na uongozi mzuri. Alipozungumza na shirika la habari la IPS, Padre Odima alisema demokrasia na uongozi bora umelikwepa bara la Afrika kwa takriban miaka 40. Matokeo yake ni kuwa Waafrika wamenyanganywa haki zao za kimsingi na viongozi walioingia madarakani kwa mtutu wa bunduki na sio uchaguzi.
Ukiukaji wa haki za binadamu barani Afrika ni kitisho kikubwa na hiyo ni changamoto kwa serikali ya Obama. Amekumbusha kuwa UKIMWI, umasikini,ufisadi,njaa,uongozi mbaya,vita vya wenyewe kwa wenyewe na ubadhilifu wa raslimali ni mambo yanayoendelea kulikaba bara la Afrika.
Kwa maoni ya Padre Odima,viongozi wa Kiafrika wahimizwe na Obama kuelekea kwenye demokrasia halisi na kukabiliana na ukiukaji wa haki za binadamu na ufisadi katika nchi kama vile Uganda,mchakato wa mageuzi nchini Kenya,mzozo wa Sudan,maafa ya nchini Somalia na Zimbabwe na vita vilivyosahauliwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Balozi Rice alipoulizwa kuhusu dhima ya Marekani nchini Somalia alisema, Washington inaunga mkono mchakato wa amani,serikali mpya ya mpito na vikosi vya Umoja wa Afrika vinavyolinda amani nchini Somalia. Marekani inataka kuona Somalia iliyo na utulivu na uwezo wa kumaliza mateso ya binadamu na serikali inayodhibiti nchi nzima na sio kuwa nchi inayotumiwa kama kambi ya magaidi wanaoshirikiana na al-Qaeda.
Kwa maoni ya Padre Odima,mkutano wa leo unampa Rais Obama nafasi ya kuwahimiza viongozi wa Kiafrika kuleta mageuzi na kuwapa matumaini wakaazi wa bara la Afrika.
Mwandishi: P.Martin/IPS
Mhariri: M.Abdul-Rahman