Obama kukutana na viongozi wa Congress
13 Januari 2015Mkutano wa rais Obama na viongozi wa baraza la wawakilishji na seneti ni wa kwanza tangu pale baraza la Congress linalodhibitiwa na chama cha Republican kufanya kikao chake cha kwanza wiki iliyopita.
Kiongozi wa maseneta wa chama cha Democratic Harry Reid , mshirika wa siku nyingi wa rais Obama katika baraza la seneti, alishushwa cheo katika uchaguzi wa Novemba mwaka jana na kuwa kiongozi wa wachache katika seneti. Kiongozi wa upinzani Mitch McConnel , ambaye ni mwiba katika upande wa Obama kama kiongozi wa wachache katika baraza la seneti , sasa amechukua wadhifa wa zamani wa Reid katika baraza hilo la juu.
Mazungumzo ya fursa za ushirikiano
Watu hao watatu watajiunga na spika wa bunge John Boehmer na kiongozi wa wabunge wa chama cha Democratic Nancy Pelosi katika ofisi ya rais kujadili fursa za uwezekano wa ushirikiano kati ya chama cha Democratic na Republican mwaka huu.
Hata hivyo haifahamiki bado kwamba vyama hivyo viwili vitaweza kufumbia macho tofauti zao za wazi katika masuala kadhaa na kuangalia katika maeneo machache ya msimamo wa pamoja.
Vyama vyote viwili vilimaliza uchaguzi wa muhula wa kati mwaka jana vikizungumzia kwa matarajio juu ya kufanyakazi kwa pamoja kuhusiana na mageuzi ya kodi, kukuza biashara na maendeleo ya miundo mbinu - maeneo ambayo Obama na Warepublican wanaweza kwa kiasi fulani kukubaliana.
Lakini mwanzoni mwa mwaka huu umetamalaki kwa kiasi kikubwa na mapambano yale ambayo yanatambuliwa kuhusiana na bomba la Keystone XL, hatua za Obama kuhusu wahamiaji pamoja na sera zake za mambo ya kigeni.
Nafasi ya maafikiano
Katika muda wa wiki mbili zilizopita, Obama mara kwa mara ametishia kuchukua hatua ya kutumia kura yake ya turufu kuzuwia miswada ambayo Warepublican wameiwasilisha kama masuala yao ya umbele.
Hata hivyo , msemaji wa Ikulu ya Marekani Josh Earnest amesema kuna " mambo chungu nzima" ambayo Obama anaweza kuyafanya mwaka huu pamoja na Warepublican.
"Haina maana tutakubaliana na kila kitu - kwa hakika hilo haliwezekani," amesema Earnest. " Lakini suala ni kwamba , tutaruhusu hali ya kutokubaliana kuhusu masuala machache na kuwa chachu cha kufikiwa makubaliano mengine yote.
"Rais anahakika kwamba hilo halitatokea," ameongeza.
Haijafahamika wazi iwapo Reid atahudhuria kikao hicho. Anapata nafuu kutokana na maumivu yanayohusiana na mazowezi na msemaji wake amekataa kusema iwapo atakuwapo katika mkutano huo.
Mwandishi : Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman