1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama - Mswada wa Marekebisho ya sekta ya fedha.

22 Julai 2010

Rais Barack Obama atia saini kuidhinisha kuwa sheria mswada wa marekebisho ya sekta ya fedha.

Rais Barack Obama,katikati,atia saini mswada wa marekebisho ya sekta ya fedha.Picha: AP

Rais wa Marekani Barack Obama hapo jana alitia saini kuidhinisha kuwa sheria marekebisho makubwa katika sekta ya fedha kuwahi kufanyika tangu miaka ya 1930 na kuahidi wananchi kuwa hawatolipishwa kwa matumizi makubwa ya serikali.

Akizungumza baada ya kuitia saini,rais Obama amesema sheria hiyo mpya itasahihisha makosa yaliotokea wakati wa mgogoro wa uchumi.

Rais Barack Obama akizungumza mjini Washington.Picha: AP

Sheria hiyo ambayo baadhi ya wanachama wa Republican wameahidi kuibatilisha inaanzisha ulinzi mpya kwa wanunuzi,inaangalia mamlaka ya benki kubwa na kuchunguza udanganyifu unaotekelezwa na kampuni za mikopo.

Katika jitihada za kurejesha imani ya uongozi wake wa kiuchumi,huku tatizo la ajira likizidi,rais Obama  amesema mgogoro wa kiuchumi ulijiri kutokana na kutowajibika kwa baadhi katika sekta ya fedha nchini humo uliopenya mpaka kwa uongozi wa nchi.

Sheria hii iliyopitishwa na bunge wiki iliyopita, ni ya pili inayoidhinishwa kuwa sheria na rais Obama baada ya ile ya marekebisho katika sekta ya afya ilioidhinishwa mapema mwaka huu.

Mswada huo wa marekebisho katika sekta ya fedha nchini Marekani, ulipitishwa bungeni kwa kura kidogo za wanachama wa Republican,huku wengine wa chama hicho cha upinzani wakishikilia azimio lao la kupinga mpango wa marekebisho wa Rais Obama kwa njia zozote zile.

Viongozi wa chama hicho cha upinzani  hapo jana waliishtumu sheria hiyo wakiitaja kusitisha ukuaji na kuekea vikwazo wafanyibiashara wakubwa nchini Marekani.

Mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya chama hicho, Michael Steele, alimlaumu rais Obama kwa kujaribu kuwashawishi Wamarekani kuwa anafanya kila awezalo katika uongozi wake, kupunguza ukosefu wa ajira.

Michael amesema Obama ametia saini sheria hiyo ambayo itakandamiza jamii ya wafanyibiashara kwa athari zisizotarajiwa,kufanya kuwa vigumu kupata mikopo  na sheria nyingine nyingi zinazouwa biashara.

Obama anakabiliwa tena na kushuka kwa uuungwaji mkono katika kura za utafiti wa maoni lakini mpango huo wa kuchunguza mabenki umependelewa na wananchi wengi.

Hatahivyo mswada huo wa marekebisho ya sekta ya fedha kama ule wa marekebisho ya sekta ya afya itachukua muda kabla ya kuanza kutekelezwa na kwa hivyo huenda isisaidie hali ya kisiasa iliyopo hivi sasa.mswada huo unaziba nyufa katika sheria  na inahitaji uwazi mkubwa na uwajibikaji kwa uwekezaji ,uwekaji rehani na ukopeshaji na pia makubaliano ya kukisia bei za mali.

Hatua hiyo imesifiwa na pia kuzua shaka kwa wanauchumi na wachambuzi.

Ambapo wengi wansema sheria hiyo inataarajiwa kuzua mjadala moto katika uchaguzi unaowadia wa bunge mwezi Novemba, huku upinzani ukitaka kuibatilisha.

Mwandishi Maryam Abdalla/AFPE

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW