1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama na Kerry kuzungumzia Mashariki ya Kati

8 Aprili 2014

Rais Barack Obama wa Marekani lanakutana na waziri wake wa mambo ya nje John Kerry kutathmini hatima ya mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati baina ya Israel na Wapalestina yanayosimamiwa na Marekani yalioko hatarini.

Rais Barack Obama wa Marekani na waziri wake wa mambo ya nje John Kerry.
Rais Barack Obama wa Marekani na waziri wake wa mambo ya nje John Kerry.Picha: Getty Images

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani aliyeonekana kuwa aliyekata tamaa wakati aliporudi Washington mwishoni mwa juma lililopita na kusema kwamba anahitaji kujadili na Obama iwapo kuendelea kutumia muda mkubwa wa wakati na mtaji wa kisiasa katika juhudi zinazodhoofishwa na pande zote mbili Israel na Marekani, yumkini leo akakabiliwa pia na masuala katika kikao cha bunge kuhusu mkakati wake kwa Mashariki ya Kati.

Maafisa waandamizi wa serikali ya Marekani wamekataa wazo kwamba Obama anakusudia kusitisha juhudi hizo na kusema kwamba anathamini sana juhudi zinazofanywa na mwanadiplomasia wake huyo mkuu.

Lakini pia inabidi Obama apate imani kwamba juhudi hizo kubwa zinazofanywa na Kerry zinastahiki,wakati kukiwa na fursa ndogo ya kufanikiwa na kuongezeka kwa mizozo ya dunia mahala kwengine kukihitaji nadhari ya Marekani.

Maamuzi magumu yahitajika

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jay Carney amesema suala sasa ni iwapo pande hizo mbili husika zinaweza kuonyesha kwamba ziko tayari kufanya maamuzi magumu ambayo yanahitajika ili mchakato huo uweze kupiga hatua.

Rais Mahmud Abbas wa Palestina na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Picha: picture-alliance/dpa

Amesema pande hizo yaani Israel na Wapalestina zinafahamu maamuzi yanayotakiwa na zinafahamu kwamba hayo sio maamuzi ambayo yanaweza kufanywa na Marekani au nchi nyengine yoyote ile.Ni maamuzi ambayo wao wenyewe tu ndio wanaoweza kuamuwa.

Kerry atakutana na Obama na Makamo wa Rais Joe Biden leo mchana katika Ikulu ya Marekani baada ya kujibu masuali bungeni. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema hapo jana usiku kwamba juhudi bado zinaendelea Mashariki ya Kati kuyaokowa mazungumzo hayo. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Jen Psaki amesema kutokana na ombi la pande hizo mbili Marekani iliandaa mkutano kati ya wajumbe wa upatanishi wa Israel na Palestina jana jioni kuendeleza juhudi nzito za kutatuwa tafauti zao.Ameongeza kusema kwamba tafauti bado zingalipo lakini pande zote mbili zimekubali kupunguza tafauti hizo

.

Maafisa mjini Jerusalem wamegoma kusema mazungumzo hayo yanafanyika wapi lakini leo yamemalizika bila ya kufikiwa ufumbuzi na imeelezwa kwamba wajumbe katika mazunguzo hayo wamekubaliana kukutana tena.

Wapalestina waonywa

Waziri wa mambo ya nje wa Israel amewaonya Wapalestina leo hii kwamba mpango wa kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina hautotekelezwa kwa kadri watakavyoendelea na kile alichokiita juhudi za uchokozi za kujiunga na mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman.Picha: Reuters

Avigdor Lieberman pia amewashutumu Wapalestina kwa kuvunja masharti ya mazungumzo hayo ya amani yanayosimamiwa na Marekani na kusema kwamba wanapaswa kugharamika kwa hilo.

Israel inataka kurefusha muda wa mwisho wa mazungumzo hayo wa tarehe 29 Aprili lakini Wapalestina watafanya hivyo ikiwa tu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu atawaachia wafungwa na kuahidi kusitisha ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu na Israel.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/AP/Reuters

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW