Obama na Merkel waapa kuiwekea vikwazo zaidi Urusi
3 Mei 2014Obama na Merkel wamekiunganisha kitisho hicho kwa uchaguzi wakati walipouhutubia mkutano wa waandishi wa habari katika ikulu ya mjini Washington baada ya kufanya mazungumzo yaliyotawaliwa na hali halisi ya mambo nchini Ukraine. Viongozi hao wamesema wameungana na kuapa kusonga mbele na hatua ya kuiwekea vikwazo vikali zaidi Urusi lakini wakatangaza wazi kwamba bado kunafanyika mashauriano kuamua jinsi ya kuviandaa vikwazo hivyo iwapo vitahitajika.
Uchaguzi wa Ukraine unalenga kumchagua mrithi wa Viktor Yanukovich, kiongozi aliyeiunga mkono Urusi ambaye alijiuzulu kufuatia maandamano ya umma na ambaye kuondolewa kwake madarakani kumechochea mzozo mbaya kabisa kati ya mashariki na magharibi tangu enzi ya vita baridi.
Katika wiki za hivi karibuni waasi wanaoiunga mkono Urusi wamezusha machafuko mashariki mwa Ukraine katika kile ambacho nchi za magharibi zinakiona kuwa ni juhudi ya rais wa Urusi, Vladimir Putin, kutaka Urusi iingilie kati kijeshi, kama ilivyotokea wakati nchi hiyo ilipoliteka eneo la Crimea mwezi Machi mwaka huu.
Maafisa wa Marekani wamesema awamu nyingine ya vikwazo inaweza kuziathiri sehemu muhimu za uchumi wa Urusi kama vile nishati, ulinzi, huduma za fedha na uhandisi. "Kama tutashuhudia machafuko na vurugu zikiendelea sana kiasi cha kuvuruga uchaguzi wa Mei 25, hatutakuwa na chaguo lengine bali kusonga mbele na kuweka vikwazo vikali zaidi," amesema rais Obama.
Marekani na washirika wake wa Ulaya wamekuwa wakifuatilia kwa umakini mkubwa mienendo ya wanajeshi 40,000 wa Urusi walioko katika mpaka wa mashariki wa Ukraine na utekaji wa majengo ya serikali katika miji ya mashariki mwa Ukraine na wanamgambo wanaoiunga mkono Urusi. Maafisa wa Marekani na Ulaya wameonya Urusi itakabiliwa na vikwazo zaidi vya kiuchumi iwapo italivamia eneo hilo.
Sekta ya nishati na benki kulengwa
Obama na Merkel wamesema wana imani uchaguzi wa Ukraine utafanyika kwa amani na kama ilivyopangwa ili taifa hilo liweze kuanza kuuimarisha upya uchumi wake. "Uchaguzi wa Mei 25 hauko mbali sana. Kama itashindikana kuiimarisha hali, vikwazo zaidi havitaepukika," amesema kansela Merkel.
Marekani na Umoja wa Ulaya tayari zimepitisha awamu kadhaa ya vikwazo dhidi ya Warusi, wakiwemo watu waliokaribu na rais Putin pamoja na kampuni kadhaa. Urusi imepuuzilia mbali vikwazo hivyo ingawa rais Obama amesema ni kipengee muhimu katika kuporomoka kwa soko la hisa la Urusi na kushuka kwa thamani ya sarafu ya Urusi. "Lengo si kuiadhibu Urusi bali kuibadili tabia yake," akaongeza kusema Obama.
Sekta ya nishati na benki ni maeneo mawili muhimu yatakayolengwa iwapo vikwazo vitaongezwa. Maafisa wa Ulaya wana wasiwasi kulilenga soko la nishati la Urusi yumkini kukaziumiza chumi za mataifa ya Ulaya yanayoitegemea gesi asilia kutoka Urusi.
Obama ameitaka Urusi kuyashawishi makundi ya wapiganaji yanayoiunga mkono nchini Ukraine yaweke chini silaha na kusema inafedhehesha kwamba waasi hao wanawazuia waangalizi wa kimataifa. Obama aidha amesema kauli ya Urusi kwamba kumetokea uasi wa wanaharakati wanaoiunga mkono Urusi mashariki mwa Ukraine imeenda kinyume na matumizi ya makombora jana Ijumaa yaliyozidungua helikopta mbili za jeshi la Ukraine.
"Ni wazi kwa ulimwengu kwamba makundi haya yanayoungwa mkono na Urusi si ya waandamanaji wa amani. Ni wanamgambo wenye silaha nzito za kisasa," akasema Obama.
Mwandishi: Josephat Charo/RTRE
Mhariri: Sudi Mnette