1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama na mkewe wamuunga mkono Kamala Harris kuwa mgombea

26 Julai 2024

Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama na mkewe Michelle leo wametangaza kumuunga mkono Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris kuwa mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha Democratic.

Kamala Harris na Barack Obama
Kamala Harris na Barack Obama.Picha: picture alliance/dpa/AP

Tangazo la Obama na mkewe Michelle la kuumuunga mkono Kamala Harris limetolewa mapema leo mchana na kuchapishwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii ya wawili hao.

Kwenye ujumbe wao ulioambatana na video inayoonesha mazungumzo ya simu kati yao na Kamala Harris, Obama na mkewe wamemweleza Harris wameridhia bila hiyana, yeye kupeperesha bendera ya chama cha Democratic katika uchaguzi wa rais wa mwezi Novemba na watamsaidia kupiga kampeni ili achaguliwe kuiongoza Marekani.

Wote wawili wamesema wanaona fahari kumuunga mkono Kamala Harris ambaye iwapo atachaguliwa kuwa rais wa Marekani atakuwa mwanamke wa kwanza kukalia kiti hicho tena aliyechanganya damu ya wamarekani weusi na asili ya kihindi.

Baba mzazi wa Kamala Harris alikuwa mhamiaji kutoka Jamaica na familia ya mama yake ni wazawa wa India.

Kamala atoa shukrani kwa familia ya Obama na kuahidi kampeni za kishindo

Kamala HarrisPicha: Brendan Smialowski/Pool/REUTERS

Kwenye mazungumzo hayo ya simu Kamala alitoa shukrani za dhati kwa familia ya Obama na kuwafahamisha kwamba yuko tayari kwa kampeni kabambe.

"Michelle (na) Barack hili lina maana kubwa sana kwangu. Ninatumai kutimiza ndoto hii pamoja nanyi.... Zaidi ya yote ningependa kusema maneno mliyoniambia na urafiki mliouonesha kwangu kwa miaka yote hii vina uzito usioelezeka. Shukrani sana sana." amesema Harris. 

Uamuzi huo wa Obama na mkewe kumuunga mkono Kamala unazingatiwa kuwa kihunzi cha mwisho kwa mwanasiasa huyo kujikatia tikiti ya kuwa mgombea urais kupitia chama cha Democratic.

Ikumbukwe Kamala atasubiri uteuzi rasmi wa chama cha Democratic kitakapofanya mkutano wake mkuu mnamo mwezi unaokuja.

Tangu rais Joe Biden alipotangaza kutowania muhula wa pili na kumpendekeza Kamala kuchukua nafasi ya kuwa mgombea, wanasiasa vigogo ndani ya chama cha democratic walijitokeza haraka haraka kusimama nyuma ya makamu huyo wa rais.

Miongoni mwao ilikuwa ni spika wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi na familia ya Obama ilikuwa ikisubiriwa kwa shauku itangaze kumuunga mkono.

Obama na mkewe Michelle ni moja ya Wanademocratic wanaoheshimika na wenye ushawishi mkubwa na mwaka 2016 na baadaye 2020 walishirika pakubwa kuwapigia kampeni Hilary Clinton na Joe Biden.

Kamala akoleza mashambulizi dhidi ya Trump na kumtaka asikimbie mdahalo 

Donald Trump na Kamala Harris.Picha: Evan Vucci/AP/dpa/picture alliance | Shawn Thew/Pool EPA/AP/picture alliance

Katika hatua nyingine Kamala Harris amekoleza moto wa kampeni yake ya mapema kwa kumshambulia Donald Trump anayetarajiwa kuwa mpinzani wake.

Akiwahutubia walimu kwenye mkutano mmoja wa kampeni, Kamala amesema anataka kuwa rais kwa dhamira ya kupigania hatma ya taifa hilo akionya kwamba ajenda ya Trump na kundi lake alilolitaja kuwa la "wanasiasa wa misimamo mikali" wanalenga kuirejesha nyuma Marekani.

Ameahidi kuwekeza nguvu kwenye sera za uchumi  zitakazolinda maslahi ya tabaka la wafanyakazi, haki za wnawake, afya kwa wote na sheria kali dhidi ya kumiliki bunduki.

Katika kile kinachooneka kwamba Kamala Harris amechagua stratejea ya mashambulizi mfano wa ile inayotumiwa na Trump, mwanamama huyo amemtupia kijembe Trump akimtuhumu kutka kukimbia mdahalo uliopangwa mwezi Septemba.

Mapema jana kikosi cha kampeni cha Trump kilesema hakiwezi kutoa jibu la uhakika iwapo Trump atashiriki mdahalo wa Septemba na Kamala Harris.

Wametoa sababu kwamba mdahalo hip ulipangwa wakati wa Biden hajajitoa katika kinyanganyiro na kwamba hadi sasa bado Harris hajathibitishwa kuwa mgombea rasmi wa Democratic.

Msimamo huo wa Trump na timu yake ya kampeni ndiyo ulimwibua Kamala aliyewaambia waandishi habari kuwa yuko tayari kwa mchuano wa mdahalo wa televisheni na kumtaka Trump asitafute sababu za kuukwepa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW