1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama na viongozi wa Ulaya waijadili NATO

Mohamed Dahman
18 Novemba 2016

Rais Barack Obama wa Marekani na viongozi wa Ulaya wasisitiza umuhimu wa kushirikiana katika Jumuiya Kujihami ya NATO na kuikaripia Urusi kwa hatua zake Syria na kushindwa kutekeleza mkataba wa amani wa Ukraine

Deutschland Sechser-Treffen mit Merkel und Obama im Kanzleramt
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Ikulu ya Marekani imetowa taarifa hiyo kufuatia mkutano huo wa Ijumaa (18.11,2016) mjini Berlin ambapo kwayo Obama alitaka kuwahakikishia viongozi wenzake wa Ujerumani, Uingereza, Uhispania,Italia na Ufaransa kwamba mrithi aliechukuwa nafasi yake Donald Trump hatovunja ushirika uliopo kati ya Ulaya na Marekani.

Trump alizusha mashaka wakati wa kampeni wakati aliposema anaweza kuzuwiya msaada wa kijeshi kwa washirika wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO iwapo washirika hao hawatotimiza ahadi zao za kijeshi pamoja na kusema kwamba atakuwa na ushirikiano wa karibu na Rais Vladimir Putin wa Urusi.

Ikulu ya Marekani imesema Rais Obama ameelezea imani yake hata katika kipindi cha mabadiliko makubwa maadili ya demokrasia yameweza kufanya kazi kubwa ya kuundeleza uhuru wa binaadamu na maendeleo kuliko mfumo wowote ule katika historia na itaendelea kufanya hivyo kwa kusonga mbele.

Viongozi hao wamekubaliana juu ya haja ya kushirikiana kuleta utulivu Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini pamoja na kufanikisha utatuzi wa kidiplomasia kwa mizozo nchini Syria na Ukraine.

Viongozi wa Ulaya wataka kuungwa mkono na Obama

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy.Picha: Reuters/F. Bensch

Viongozi wa Ulaya walikuwa wakitaka kuungwa mkono na Obama wakati wakijiandaa kurefusha vikwazo dhidi ya Russia vilivyowekwa na Marekani na Umoja wa Ulaya hapo mwaka 2014 kufuatia kuingilia kati kwake mashariki mwa Ukraine na wanafikiria kuweka vikwazo vipya kuhusiana na hatua za Russia nchini Syria ambapo inamuunga mkono Rais Bashar al- Assad.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani katika mkutano na waandishi wa habari uliohudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy amesema hakuna uamuzi uliofikiwa juu ya kurefusha vikwazo kuhusiana na suala la Ukraine lakini hatua zitachukuliwa iwapo makubaliano ya amani ya Minsk yatakaposhindwa kukidhi haja.

 Merkel amesema "Tumejadili Syria kwa kina na kusema kabla ya yote hali ya kibinaadamu huko Allepo lazima iboreshwe.Hatukujadili mahsusi vikwazo dhidi ya Russia kuhusiana na suala hilo.Tumejadili vikwazo kuhusiana na Ukraine.Tunataka kuhakikisha tunapiga hatua na mchakato wa Minsk ambapo kwa bahati mbaya hadi sasa hatukuona maendeleo makubwa."

Kansela Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May.Picha: Reuters/M. Sohn

Russia yahofiwa kufanya mashambulizi mapya Syria na Ukraine

Viongozi wa Umoja wa Ulaya walitegemea kurefusha vikwazo hivyo mwezi wa Disemba au Januari kabla ya kumalizika muda wake hapo mwezi wa Januari.

Merkel pia amesema hawakujadili suala la kuiwekea Russia vikwazo kuhusiana na hatua  yake ya kuishambulia Syria kwa mabomu kumsaidia rais Assad wa nchi hiyo.

Viongozi wa Ulaya walikuwa wakihofu kwamba Russia itatumia muda huu kabla ya kuapishwa kwa Trump hapo mwezi wa Januari kufanya mashambulizi mapya nchini Syria na Ukraine.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ Reuters

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW