Obama: Tulikadiria vibaya uwezo wa IS
29 Septemba 2014Mashambulizi ya anga yaliyofanywa usiku wa kuamkia leo dhidi ya kundi hilo lijulikanalo kama Dola la Kiislamu, au IS, yamejikita katika mikoa miwili ya Raqa na Aleppo ambayo ni ngome muhimu za kundi hilo, hii ikiwa ni kwa mujibu wa shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria ambalo lina makao yake makuu nchini Uingereza.
Shirika hilo limesema kwamba miongoni mwa vituo vilivyolengwa ni pamoja na kiwanda cha kusindika nafaka katika mji unaoshikiliwa na Is wa Minbej, ambacho kilikuwa kikiendeshwa na raia wa kawaida. Mkuu wa shirika hilo Rami Abdel Rahman amesema wanazo taarifa kuwa raia wameuawa katika shambulizi hilo, lakini hakuthibitisha idadi ya wahanga.
Shabaha nyingine ya mashambulizi ya usiku wa leo ilikuwa makao makuu ya kimkoa ya Dola la Kiislamu yaliyo kati ya mji wa Minbej na Jarabulus ambao uko kaskazini zaidi. Katika mkoa wa Raqa, ndege za Marekani na washirika wake zimeshambulia kizuizi cha barabarani, nje kidogo ya ya mji wa Raqa ambao ndio makao makuu ya kundi hilo.
Makadirio mabaya
Huku mashambulizi hayo yakiendelea, rais wa Marekani Barack Obama amesema kupitia mazungumzo na kituo kimoja cha televisheni nchini Marekani, kwamba walikuwa na makisio yasiyo sahihi kuhusu uwezo wa kundi hilo.
''Mkuu wa taasisi zetu za ujasusi Jim Clapper ameekiri kwamba makadirio yao juu ya kile kinachofanyika nchini Syria yalikuwa ya chini.'' Amesema Obama.
Obama alisema kuwa wapiganaji wa kijihadi waliofurushwa kutoka Irak kabla ya majeshi ya Marekani kuondoka mwaka 2011, wote walihamia nchini Syria, na kwamba kwa msaada wa makabila ya madhehebu ya Suni wameweza kujikusanya na kuunda kundi hatari zaidi la IS.
Uwezo wa jeshi la Irak
Hali kadhalika rais Obama alikiri katika mazungumzo hayo na kituo cha Televisheni, kuwa Marekana ilijidanganya kwa makadirio ya uwezo wa Irak kukabiliana na kundi hilo.
Maeneo mengine yalipigwa katika mashambulizi ya jana ni pamoja na mji wa Tal Abyad ulio karibu na mpaka baina ya Syria na Uturuki, ambako shule inayotumiwa kuwahifadhi wanamgambo imepigwa.
Kabla ya mashambulizi haya ya karibuni, ndege za washirika wa Marekani zililiharibu lango la mtambo mkubwa zaidi wa gesi nchini Syria mashariki mwa mji wa Deir Ezzor, katika kile kilichochukuliwa kama onyo kwa wanamgambo wa IS wanaokishikilia kuwataka wahame.
Mtambo huo huvihudumia vituo kadhaa vya umeme katika mkoa wa Homs unaodhibitiwa na serikali, na ikiwa kitaacha kufanya kazi mikoa kadhaa itabaki bila umeme.
Mwandishi: Daniel Gakuba/APE/RTRE/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef