1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama : Ulaya iwajumuishe vyema Waislamu

17 Januari 2015

Rais Barack Obama wa Marekani amezihimiza serikali za Ulaya kujaribu kuwajumuisha vyema Waislamu walio wachache katika jamii wakati ikikabiliana na mashambulizi ya kigaidi kama yale yaliotokea mjini Paris wiki iliopita.

Rais Barack Obama wa Marekani na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameroon wakiwa katika Ikulu ya Marekani.
Rais Barack Obama wa Marekani na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameroon wakiwa katika Ikulu ya Marekani.Picha: picture-alliance/epa/O. Douliery

Katika mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani Ijumaa (16.01.2015) akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ambaye ni mgeni wake wa kwanza kutoka nje tokea kuzuka kwa mauaji katika ofisi ya jarida la Charlie Hebdo mjini Paris wiki iliopita Obama amesema nchi washirika zitasimama pamoja na Ufaransa.

Lakini pia ameonya kwamba jibu la kukabiliana na mashambulizi hayo lisiwe tu msako wa kiusalama.

"Najuwa David anaungana nami wakati ninaposema tutaendelea kufanya kila tuwezalo kuisadia Ufaransa kupata haki inayohitajika na kwamba nchi zote zinashirikiana bila ya vikwazo kuzuwiya mashambulizi na kuyashinda makundi hayo ya kigaidi" amesema Obama.

Obama amesema mashambulizi hayo ya Paris "yanaonyesha jinsi makundi ya kigaidi kama vile Al Qaeda na ISIL yanavyojaribu kwa vitendo kuchochea na kuwaunga mkono watu waliomo ndani ya nchi zetu ili wajihusishe na ugaidi."

Kujumuishwa kwa jamii za wachache

Kiongozi huyo wa Marekani amesema miripuko katika Mbio ndefu za Marathon za Boston mwaka 2013 imeonyesha kwamba Marekani haiko salama kabisa kutokana na makundi ya kijihadi lakini amesema kwamba ilikuwa na mafanikio zaidi kuliko nchi nyengine katika kuwajumuisha katika jamii watu wa makabila ya wachache.

Msikiti wa Waturuki wa Sehitlik ulioko katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin.Picha: Getty Images/A. Rentz

Amesema fursa yao kubwa ni kwamba wananchi wao Waislamu wenyewe wanajihisi kuwa ni Wamarekani na kuna mchakato mzuri wa uhamiaji na kujumuishwa katika jamii ambao ni sehemu ya mila yao.

Kwa mujibu wa Obama amesema kuna sehemu za Ulaya ambapo hali haiko hivyo na kwa hiyo ni muhimu kwa Ulaya sio tu kukabiliana na hali hiyo kwa kutumia nyundo,polisi na jeshi kushughulikia matatizo hayo.

Ameongeza kusema kwamba inabidi pia kuwepo na utambuzi kwamba ni muhimu kwa kadri uhusiano unavyokuwa madhubuti na Afrika Kaskazini au Wafaransa wenye asili ya Afrika kaskazini kwa uhuru wa Ufaransa.

Washirika madhubuti

Amesema David na Uingereza zinaendelea kuwa washirika madhubuti katika kazi hiyo ikiwa ni pamoja kushirikiana ujasusi na kuimarisha usalama wa mipakani.

Rais Barack Obama wa Marekani na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameroon wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani. (16.01.2015)Picha: Reuters/L. Downing

Marekani itaandaa mkutano wa kilele hapo mwezi wa Februari juu ya kukabiliana na matumizi ya nguvu ya makundi ya itikadi kali na tishio la wapiganaji wa Kiislamu waliopandikizwa mawazo ya itikadi kali wanaorejea nyumbani kutoka vitani nchini Syria.

Cameron amesema wamekubaliana kuunda timu ya pamoja kutambuwa kitu gani zaidi wanaweza kufanya kupambana na kuongezeka kwa matumizi ya nguvu ya watu wa itikadi kali na kila mmoja kujifunza kutoka mwenzake.

Vitisho kwa utengamano

Ameyaelezea mapambano yanayozikabili serikali za mataifa ya magharibi kuwa yatadumu kwa muda mrefu, yanahitaji subira na magumu na kumueleza adui kuwa ni mlokole alie na sumu mwenye uchu na vifo na ambaye anaipotosha dini ya Uislamu.

Marekani na Uingereza tayari zinashirikiana kwa karibu katika uchunguzi kwa njia ya elektroniki duniani na Cameron amesema wamekubaliana pia kuimarisha ushirikiano wao katika suala la usalama wa mtandao.

Katika taarifa tafauti Ikulu ya Marekani imesema Shirika la Upelelezi la Marekani FBI litaunda kitengo cha pamoja cha usalama wa mtandao na shirika la ujasusi wa ndani ya nchi M15 pamoja na shirika la udukuzi GCHQ.

Ulinzi waimarishwa nchini kote Ubelgiji baada ya kuzimwa kwa jaribio la kigaidi la kuwashambulia askari.Picha: picture-alliance/dpa/Nicolas Maeterlinck

Kwa mujibu wa viongozi hao hatua hiyo itaharakisha kushirikiana taarifa za ujasusi na kuimarisha ulinzi wa nchi washirika dhidi ya mashambulizi ya mtandaoni kutoka serikali za kigeni na wahalifu.

Katika wiki za hivi karibuni serikali ya Marekani imekarahishwa kutokana na kunyakuliwa kwa akaunti ya kijeshi ya mtandao wa Twitter na wafuasi wa kijihadi na kughadhabishwa na madai ya kushambuliwa kwa mtandao wa kampuni ya filamu ya Marekani ya Sony.

Obama mwenye umri wa miaka 53 anamalizia kipindi chake cha mwisho cha miaka miwili madarakani wakati Cameron mwenye umri wa miaka 48 anajiandaa kwa uchaguzi mkuu hapo mwezi wa Mei ambao unatarajiwa kuwa wa mchuano mkali na unaweza ukawa ndio mwisho wa serikali yake ya mseto.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Caro Robi