1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama: Wakati wa mpito ni sasa

Sekione Kitojo2 Februari 2011

Rais Barack Obama wa Marekani amemwambia Rais Hosni Mubarak wa Misri jana kuwa utaratibu wa kipindi cha mpito kukabidhi madaraka nchini humo unapaswa kuanza sasa.

Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: AP

Jamii ya kimataifa inaendelea kutiwa wasiwasi na hali ya kisiasa nchini Misri na wanasisitiza kuwa muda huu wa mpito sharti uwe wa amani. Rais Barack Obama wa Marekani amemwambia rais Hosni Mubarak wa Misri jana kuwa utaratibu wa kipindi cha mpito kukabidhi madaraka nchini humo unapaswa kuanza sasa.Hayo yalikuwa matamshi ya kukosoa mpango wa kiongozi huyo wa Misri wa kubakia madarakani kwa muda wa miezi mingine sita.

"Kile ambacho ni wazi, na kile ambacho nimemweleza rais Mubarak ni imani yangu kuwa utaratibu mzuri wa hatua za mpito unapaswa kuwa wenye manufaa, na unapaswa kuwa wa amani , na hatua hizo zinapaswa kuanza hivi sasa."

Rais Hosni Mubarak akilihutubia taifa Ijumaa iliyopitaPicha: dapd

Rais Obama alizungumza na Mubarak kwa muda wa nusu saa kwa simu baada ya mshirika huyo wa siku nyingi wa Marekani kutangaza mpango wa kung'atuka kutoka madarakani mwezi Septemba mwaka huu, na kwamba hatagombea tena wadhifa huo kutokana na maandamano makubwa ya kuupinga utawala wake wa miaka 30 nchini humo yaliyofanyika katika miji kadha.

Afisa wa ngazi ya juu wa utawala wa Marekani amesema kuwa , mazungumzo ya Obama na Mubarack yalikiwa ya uwazi na moja kwa moja na hayakuacha shaka kuwa muda wa mpito ni sasa, hauwezi kuzimwa.

Umma kwenye uwanja wa TahrirPicha: picture-alliance/dpa

Amesema inafahamika ni kiasi gani Mubarak anaipenda nchi yake, na ni kiasi gani hali hii ni ngumu kwake. Rais Obama amemweleza kuwa hatua za mpito zilizo katika utaratibu mzuri haziwezi kurefushwa, zinapaswa kuanza sasa.

Wakati Marekani inashaka kuwa tamko la Mubarak la kutogombea tena wadhifa wa urais litawaridhisha waandamanaji , maafisa wamekuwa wakisita kuweka mbinyo wazi wa yeye ajiuzulu na kuepuka kuwatumbukiza washirika wengine katika eneo hilo katika mzozo kama unaotokea nchini Misri.

Obama kwa kiwango kikubwa ameiweka Marekani upande wa waandamanaji wanaodai mageuzi ya kidemokrasia , kijamii na kiuchumi nchini Misri, mshirika wa siku nyingi wa Marekani katika eneo la mashariki ya kati. Obama amesema si jukumu la nchi yeyote kumchagua kiongozi wa Misri. Ni watu wa Misri tu ndio wanaoweza kufanya hivyo.

"Kwa watu wa Misri, hususan vijana wa Misri, nataka nieleweke wazi. Tunasikia sauti zenu. Sina shaka yeyote kwamba mtaamua mustakbali wenu."

Kutokana na hali ya mambo inavyokwenda kasi, changamoto kwa Obama ni kuepuka kumtenga yeyote atakayeingia madarakani nchini Misri, kutokana na jukumu lake katika hatua za amani katika mashariki ya kati pamoja na udhibiti wa njia muhimu ya kupitisha mafuta katika mfereji wa Suez.

Nae rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, amesema leo kuwa anataka kuona hatua za kisiasa za mpito nchini Misri zifanyike bila kuchelewa.

Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani ambaye yuko ziarani nchini Israel , amesema kuwa Israel haipaswi kujificha nyuma ya machafuko nchini Misri na kusitisha juhudi za kufikia makubaliano ya amani na Wapalestina.

Hali ya ghasia na maandamano nchini Misri imekuwa ni mada kuu katika mazungumzo baina ya Bibi Merkel na viongozi wa Israel jana, ambapo rais wa Israel, Shimon Peres, ameonya kutokea uwezekano wa kuingia madarakani kwa udikteta wa kidini nchini humo.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre/afpe

Mhariri: Othman Miraj.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW