1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama ziarani Ujerumani

Isaac Gamba
16 Novemba 2016

Rais Barack Obama anaendelea na ziara yake ya mwisho barani Ulaya kabla ya kuondoka madarakani kwa kuizuru Ujerumani, nchi ambayo imekuwa daima ikimpokea kwa mikono miwili na kuwa naye karibu kwenye mengi.

Deutschland Barack Obama Rede vor dem Brandenburger Tor in Berlin
Picha: picture-alliance/dpa/K. Niefeld

Kuna wakati ambapo Rais Obama alichukuliwa kama nyota wa muziki  nchini Ujerumani. Ilikuwa wakati  wa majira ya kiangazi mnamo mwaka 2008 wakati  alipozuru Ujerumani na kabla ya kuchaguliwa kuwa rais ambapo zaidi ya watu 200,000 walikusanyika katikati ya jiji la Berlin kushuhudia kiongozi huyo akihutubia. 

Kansela Merkel hajawahi kuruhusu mgombea wa nafasi ya rais kufanya  mikutano yake katika eneo hilo maarufu, lakini ni mara chache sana eneo hilo liliruhusiwa kutumika kwa ajili ya hafla ya viongozi wakuu wa nchi.  

Ilikuwa pengine ni hatua ya awali kati ya Merkel na Obama aliyetarajiwa wakati huo kuwa rais wa baadaye wa Marekani kuanzisha mahusiano ya kisiasa.  

Mara tu baada ya kushika rasmi madaraka ya uongozi kama rais wa Marekani, Wajerumani walimuunga mkono kwa kiwango kikubwa. 

Mtangulizi wake, George W. Bush, alikuwa tayari amechukiwa kutokana na vita vya Afghanistan na Iraq ambapo wakati alipokuwa akikaribia kumaliza muda wake wa uongozi ni asilimia 14 tu ya Wajerumani walikuwa na imani na uwezo wake katika kushughulikia masuala ya kidunia.  

Rais Obama alileta matumaini mapya katika uhusiano kati ya Ujerumani na Marekani ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kukomesha migogoro. 

Obama kipenzi cha Wajerumani

Katika mwaka wake wa kwanza, asilimia 94 ya Wajerumani walionesha kumuamini kutokana na kuifanya Marekani  kwa mara nyingine kuwa mshirika wa kimataifa.

Rais Barack Obama (kushoto) alikaribishwa mwaka 2013 na Kansela Angela Merkel, na daima wawili hawa wamekuwa marafiki wakubwa na wa karibu.Picha: picture-alliance/dpa/EPA/M. Sohn

"Mahusiano na bara la Ulaya yamekuwa bora zaidi katika kipindi chake cha uongozi", anasema Jurgen Trittin, mjumbe Kamati ya Mambo ya Nje na mbunge wa chama cha Walinzi wa Mazingira alipozungumza na DW.

Watu walio karibu na wanasiasa hao wanasema Obama na Merkel wanaonekana kufanana  katika masuala kadhaa ya kisiasa, huku uhusiano wa kisiasa kati ya viongozi hao ukizidi kukua na viongozi wa Marekani  wakimsifia Kansela Merkel kutokana na hatua madhubuti alizochukua juu ya wakimbizi, ikiwa ni pamoja na kufungua milango na kuruhusua wakimbizi kiasi cha 800,000 kuingia nchini Ujerumani mwaka jana. 

"Huu ni uhusiano muhimu sana ambao nimekuwa nao, Kansela Merkel ni mtu anayeaminika ni mtu ambaye anasimamia maamuzi yake na ndio maana amekuwa kiongozi bora kwa muda mrefu kwa vile anasimamia na kutekeleza kile anachokisema," anasema Trittin.

Wakati wa kipindi cha miaka minane kama viongozi wa mataifa yao mawili, Rais Obama na Kansela Merkel wamekuwa msingi wa mahusiano kati ya nchi za Ulaya na Marekani, licha ya changamoto zilizotokana na kashifa  iliyoibuka mwaka 2013 ambapo ilibainika mashirika ya kijasusi ya Marekani yalikuwa yakifuatilia na kukusanya taarifa kwa njia ya siri zilizowahusu raia wa Ujerumani pamoja na kuitega simu ya mkononi ya Kansela Merkel na kusikiliza mazungumzo yake kupitia simu hiyo. 

Hali hiyo ilidhoofisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili katika kipindi hicho hadi pale Mkuu wa Utumishi katika ikulu ya Marekani alipozuru Ujerumani kwa ajili ya kutuliza mvutano. 

Aidha suala jengine ambalo linaonekana kutokidhi matarajio ya Wajerumani katika kipindi cha utawala wa Rais Obama ni kushindwa kwake kulifunga gereza la Guantanamo nchini Cuba licha ya kuahidi kufanya hivyo. 

Pamoja na ukosoaji huo, bado Wajerumani walishindwa kuzuia hisia zao  kuonekana kusitushwa na ushindi wa Trump katika kinyang'anyiro cha kuwania urais nchini humo kufuatia uchaguzi uliofanyika Novemba 8.

Wajerumani walitarajia mgombea wa chama cha Democrat, Hillary Clinton, kushinda nafasi hiyo na hivyo kuwa na mshirika wa kweli wa Ujerumani katika ikulu ya Marekani.

Mwandishi: Isaac Gamba/DW
Mhariri: Gakuba Daniel

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW