Obama ziarani Ulaya
3 Juni 2014Obama ameanza ziara yake hii kwa kukutana na Rais Bronislaw Komorowski wa Poland katika uwanja wa ndege wa Warsaw. Baadaye alipangiwa kuwatembelea wanajeshi wa kikosi cha anga cha Marekani na Poland kabla ya kuwa na mkutano wa pamoja na waandishi habari baada ya mazungumzo.
Akiwa Poland, nchi ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO inayopakana na Ukraine, Obama atakutana na viongozi kadhaa akiwemo rais mpya wa Ukraine, Petro Poroshenko, ambaye ataonana na Obama hapo kesho, huku Obama akitarajiwa kujibu malalamiko ya kwamba hajachukua hatua za kutosha dhidi ya Urusi baada ya kulitwaa jimbo la Crimea mwezi Machi. Kwa upande wake, Poroshenlo ameanza harakati za kidiplomasia juma hili kuhusiana na mzozo wa nchi yake.
Obama na viongozi wengine wa nchi za Magharibi wako mjini Warsaw kuhudhuria kuadhimisha miaka 25 tangu Poland ijitowe kwenye ukoministi na miaka sabini tokea siku ambapo majeshi ya nchi nne shirika, Marekani, Urusi, Uingereza na Ufaransa yalipofanya uvamizi ulioleta ushindi wakati wa vita vya pili vya dunia.
Pia atakuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu Donald Tusk ambayo pia yatahusiana zaidi na mzozo wa Ukraine.
Ahadi ya Marekani
Katika hotuba yake fupi baada ya kuwasili, Obama alikumbusha ahadi ya kujitolea kwa Marekani katika usalama wa Poland.
"Wakati wa ziara yangu hapa miaka mitatu iliyopita, nilisema Marekani itaimarisha kujitolea kwake kwa usalama wa Poland na Marekani inaheshimu ahadi yake hiyo ambayo mnaiona katika kuwepo kwa kikosi cha anga na ni jambo ambalo ni muhimu hasa katika kipindi hiki."
Mnamo siku ya Ijumaa, Rais Obama anatarajiwa kuonana na Rais Vladimir Putin wa Urusi huko Normandy, Ufaransa, katika sherehe za ushindi wa vita vya pili vya dunia.
Huo utakuwa mkutano wa kwanza wa ana kwa ana kati ya viongozi hao tangu kuzuka kwa mvutano kati yao juu ya kuhusika kwa Urusi na matukio ya nchini Ukraine.
Hali mbaya mashariki mwa Ukraine
Ripoti kutoka mashariki mwa Ukraine zinasema waasi wanaopigania kujitenga wakiungwa mkono na Urusi wameripoti kwamba raia mmoja aliuwawa katika hujuma za ndege za kivita na helikopta kusini mwa mji unaodhibitiwa na waasi hao wa Sloviansk.
Hata hivyo, maafisa wa Ukraine mjini Kiev wamekanusha wakisema hakuna mashambulizi yoyote yaliyofanyika.
Kwa upande mwengine, mawaziri wa ulinzi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO wanatarajiwa kuzingatia hatua ya muda mrefu kuhusiana na mzozo wa Ukraine. NATO imefanya luteka ya kijeshi na kuongeza shughuli za jeshi la majini na anga katika mataifa ya Baltic, Bahari Nyeusi na nchini Poland.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/Reuters/AP
Mhariri: Mohamed Khelef