1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaondoa vikwazo vya mauzo ya silaha

Sylvia Mwehozi23 Mei 2016

Katika siku ya kwanza ya ziara yake Obama amethibitisha kuondolewa kwa vikwazo vya mauzo ya silaha kwa Vietnam, vikwazo ambavyo vimedumu kwa muda mrefu.

Vietnam Besuch US-Präsident Barack Obama
Picha: Reuters/Kham

Rais wa Marekani Barack Obama yuko ziarani nchini Vietnam katika kuimarisha mahusiano baina ya mataifa hayo. Katika siku ya kwanza ya ziara yake Obama amethibitisha kuondolewa kwa vikwazo vya mauzo ya silaha kwa Vietnam, vikwazo ambavyo vimedumu kwa muda mrefu.

Kauli hiyo ya Obama aliyoitoa mwanzo wa ziara yake ya siku tatu nchini Vietnam inatajwa kuhitimisha miongo kadhaa ya marufuku ya kuuza silaha nchini humo na kwamba itaimarisha mahusiano na taifa hilo muhimu katika ukanda huo.

Katika mkutano na waandishi wa habari Obama amesema kuondolewa kwa marufuku hiyo kunamaanisha kuweka pembeni historia mbaya na taifa hilo lililokuwa adui katika vita baridi na Marekani.

"Ninaweza kutangaza kwamba , Marekani inaondoa kabisa vikwazo vya mauzo ya vifaa vya kijeshi kwa Vietnam ambavyo vimekuwepo kwa miaka 50. Kama ilivyo kwa washirika wengine, mauzo yatapaswa kukidhi mahitaji, ikiwemo yale yanahusu haki za binadamu"amesema Obama.

Ameongeza kwamba mauzo ya silaha yataangaliwa kwa undani zaidi. Mabadiliko hayo yataiwezesha Vietnam kuwa na uwezo kamili wa kupata silaha inazohitaji ili kujilinda.

Obama anataka kuweka usawa na taifa la Vietnam ambalo ameliita kuwa umuhimu katika ukanda huo, katika wakati ambao China inajaribu kukuza mgogoro katika bahari ya kusini mwa China."Katika hatua hii, pande zote mbili zimejenga imani na ushirikiano, ikiwemo majeshi yetu, ikiashiria maslahi ya pamoja na kuheshimiana" alisema rais Obama.

Obama amesema Marekani na Vietnam zote zina wasiwasi sawa juu ya masuala ya bahari na umuhimu wa kulinda uhuru wa kutumia bahari hiyo ya kusini mwa China.

Amesema ingawa Marekani haichukui upande wowote katika mgogoro huo wa umiliki, bado inaunga mkono usuluhishi wa kidiplomasia na sio nani mkubwa kumzidi mwenzake.

Kuondolewa kwa vikwazo hivyo vya uuzaji silaha kunaonekana kama jambo jema kwa viongozi wa Vietnam katika kukabiliana na fujo zinazofanwa na China. Rais wa Vietnam Tran Dai Quang amesifu kupanuka kwa ushirikiano wa kiusalama na biashara kati yake na kile alichookita"adui wa zamani aliyegeuka kuwa rafiki"na kuomba uwekezaji zaidi wa Marekani nchini mwake.

Meli ya ulinzi ya China ikipita kilometa chache kutoka VietnamPicha: Reuters

Hata hivyo wabunge na wanaharakati nchini Marekani wanamtaka Obama awashinikize viongozi wa taifa hilo la kikomunisti juu ya kuruhusu uhuru kabla ya kuondoa vikwazo hivyo. Vietnam inawashikilia karibu wafungwa 100 wa kisiasa.

Obama amesema mataifa haya yote yana mitazamo tofauti juu ya suala la haki za binadamu lakini kuna mabadiliko yanayoweza kufanywa na Vietnam.

Kimsingi Marekani iliondoa sehemu ya vikwazo hivyo mnamo mwaka 2014 lakini Vietnam ilitaka kuondolewa kamili kwa vikwazo hivyo inapojaribu kupambana na China katika mgogoro wa umiliki eneo na ujenzi wa kituo cha jeshi katika eneo la bahari.

Baada ya ziara yake nchini humo, Obama ataelekea nchini Japan kwa mkutano wa kimataifa na kuutembelea mji wa Hiroshima, ulioharibiwa kwa bomu la Nyuklia la Marekani wakati wa vita vya pili vya dunia 1945.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW