1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obrador ashinda urais Mexico

2 Julai 2018

Mgombea wa siasa za mrengo wa kushoto nchini Mexico Andres Manuel Lopez Obrador amepata ushindi mkubwa baada ya kuchaguliwa kuwa rais kwa asilimia 53 ya kura, tume ya uchaguzi imearifu.

Mexico -  Andres Manuel Lopez Obrador zum neuen Präsident gewählt
Picha: Reuters/G. Tomasevic

Mgombea wa siasa za mrengo wa kushoto nchini Mexico Andres Manuel Lopez Obrador amepata ushindi mkubwa baada ya kuchaguliwa kuwa rais kwa asilimia 53 ya kura, tume ya uchaguzi imearifu. Matokeo hayo ya awali yamezingatia idadi ya kura zilizokusanywa kutoka kwa wawakilishi kwenye vituo 7,800 vya kupigia kura. 

Rais wa taasisi ya kitaifa ya uchaguzi Lorenzo Cordova amethibitisha matokeo hayo. Amesema, Lopez Obrador ameshinda kwa kati ya asilimia 53 na 53.8 ya kura zote, wakati mgombea wa chama cha kihafidhina wa sera za wastani, Ricardo Anaya akipata wingi wa kura wa hadi asilimia 22.8, na Jose Antonio Meade anayetokea chama cha rais anayeondoka madarakani Enrique Pena Nieto cha Institutional Revolutionary, PRI akiambulia hadi asilimia 16.3 tu ya kura zote.

Baada ya matokeo hayo, Lopez Obrador alizungumza na wafuasi wake akitoa mwito kwa Wamexico wote kupatana na kuweka kando maslahi binafsi, huku akiahidi kuimarisha uhuru kwenye maeneo mbalimbali.

Kuchaguliwa kwa Obrador, kunaashiria sasa taifa hilo la kihafidhina, linageukia sera za mrengo wa kushoto na huenda kutatuliza zaidi mahusiano kati yake na Marekani, lakini pia kuwa mgombea wa kwanza wa urais kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura, tangu chama cha PRI kilipopoteza nafasi ya ushawishi yake muongo uliopita.

Wapiga kura waliojitokeza kwa wingi, wameonekana kuchoshwa na ukuaji mdogo wa uchumi na kuongezeka kwa uhalifu nchini humo.Picha: Reuters/G. Graf

Wapiga kura waliojitokeza walikadiriwa kufikia asilimia 63, kati ya raia milioni 89 walio na vigezo vya kupiga kura, ikiwa ni idadi ya juu zaidi kuwahi kutokea nchini humo.

Mgombea aliyeshindwa kwenye uchaguzi huo Ricardo Anaya, aliyegombea kupitia muungano ulioongozwa na chama cha PAN, amekubaliana na matokeo hayo ya uchaguzi uliofanyika jana Jumapili, na kuungana na wapinzani wenzake kumpongeza kwa ushindi huo. 

Rais wa Marekani, Donald Trump amempongeza Obrador kwa ushindi huo aliouita wa kishindo akisema, ana matarajio makubwa ya kushirikiana na kiongozi huyo. Ameandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba kuna mengi yanayotakiwa kufanyika kwa ajili ya maslahi ya Marekani na Mexico. Mahusiano kati ya mataifa hayo, yalifikia kiwango cha chini zaidi kufuatia sera za Trump za kupinga uhamiaji.  

Rais wa Bolivia, Evo Morales ambaye pia mfuasi wa siasa za mrengo wa kushoto, naye ameandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba wana uhakika kwamba serikali ya Obrador itaandika historia mpya kuhusu hadhi ya Amerika ya Kusini na uhuru wake.

Waziri mkuu wa Canada, amempongeza Obrador kwa ushindi huo, na kuahidi ushirikiano zaidi baina ya mataifa hayo yenye mahusiano ya karibu katika sekta ya biashara na uchumi.

Mwandishi: Lilian Mtono/dpae/afpe/.

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW