1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Odinga adai njama ya wizi wa kura Kenya

27 Januari 2017

Miezi saba kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Kenya, kiongozi wa upinzani Raila Odinga ameituhumu serikali ya Jubilee kwa kuendeleza ufisadi wa hali ya juu na kupanga njama ya kuiba kura kwenye uchaguzi huo.

Raila Odinga ARCHIV Trauer
Picha: Till Muellenmeister/AFP/Getty Images

Akizungumza na waandishi habari katika mji mkuu wa Nairobi siku ya Ijumaa, Raila Odinga, kiongozi wa muungano wa vyama vya upinzani NASA, alidai kuwa serikali ya Uhuru Kenyatta inapora mali ya umma wakati ambapo anahisi kwamba huenda ikashindwa kwenye uchaguzi ujao.

"Nilipozungumzia kashifa ya "NYS" walisema nawaonea wivu juu ya maendeleo wanayofanya, nilipozingumzia kashifa ya "Eurobond" wakatisha kuniweka kuzuizini na hatimaye hata mkaguzi mkuu wa mahesabu anasema hajaona fedha hizo kwenye vitabu vya mahesabu katika Benki Kuu,” alisema  Odinga.

Kuhusu zoezi la kusajili wapiga kura ambalo ni la mwisho kabla uchaguzi mkuu kufanyika, kiongozi huyo wa upinzani alidai kuwa serikali inatumia maafisa wa utawala kuhimiza usajili katika ngome za jubilee. Raila alisema maafisa hao hao katika ngome za upinzani wanatishwa dhidi ya kufanya hivyo.

Rais Uhuru Kenyatta atakiongoza chama cha Jubilee katika uchaguzi mkuu hapo mwezi Agosti, unaotarajiwa kuwa wa ushidani mkali.Picha: Getty Images/A.Shazly

Viongozi wa chama tawala cha Jubilee hata hivyo wameyapuuza madai ya Raila. "Ati anasema kuzunguka kwangu kuomba watu wajiandikishe, ni kuiba kura. Hiyo siasa ya vitisho tuache, watu wakitaka tushindane, tushindane kwa sera na yeye awaambie watu ni atawafanyia," alisema Rais Kenyatta katika mmoja ya mikutano yake.

Uandikishaji wapigakura waendelea

Hayo yanaendelea huku zoezi la kusajili wapiga kura ambayo ni awamu ya mwishi likiingia wiki ya pili sasa. Kila upande unafanya kampeni ya kushawishi wapiga wananchi katika ngome zao kujisajili kama wapiga kura huku Tume ya Uchaguzi IEBC ikisema haitaongeza muda wa usajili.

"Hatuoni tukiongeza muda huu kwa hivyo ikiwa hutajisalili wakati huu hutaweza kushiriki kwenye uchaguzi,” alisema mkurugenzi wa IEBC Ezra Chiloba.

Tume ya uchaguzi inalenga kusajili wapigakura wapya wapatao milioni 6 ingawaje kufikia sasa ni takriban wapiga kura milioni moja pekee waliosajiliwa.

Uchaguzi mkuu ujao unaelekea kuwa kati ya mafahari wawili, Rais Uhuru Kenyatta wa Chama cha Jubilee anayetetea kiti chake na mgombea wa muungano mpya wa upinzani wa National Super Alliance, NASA ambao mgombea wake bado hajatangazwa. Zaidi ya vyama 15 vya upinzani vimeungana na muungano wa CORD kubuni muungano mpya wa NASA.

Mwandishi: Alfred Kiti - DW Nairobi

Mhariri: Saumu Ramadhan Yusuf

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW