Odinga aongoza dhidi ya Kibaki
29 Desemba 2007NAIROBI
Mgombea urais wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga leo amekuwa akiongoza katika mchuano wa uchaguzi wa kuwania kuliongoza taifa hilo kubwa la kiuchumi la Afrika Mashariki uchaguzi ambao umeshuhudia kubwagwa kwa mawaziri kadhaa wa serikali.
Wakati kuhesabiwa kwa kura kukiingia siku yake ya tatu huku kukiwepo malalamiko ya mchakato huo kuwa wa taratibu mno Odinga amekuwa mbele dhidi ya Rais Mwai Kibaki ambaye marafiki wake wengi wameanguka kwenye chaguzi za kuwania ubunge.
Kufikia saa nane za usiku Tume ya Uchaguzi nchini Kenya imetowa matokea kutoka vituo vya uchaguzi 80 kati ya vituo 210 vya nchi nzima na kuonyesha kwamba Odinga alikuwa akiiongoza kwa kura 1,884,096 dhidi ya 1,516,219 za Kibaki.
Vituo vitatu vya televisheni nchini humo vimetowa nusu ya matokeo yakionyesha Odinga akiwa mbele sana dhidi ya Kibaki.