1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta amburuza Odinga mahakamani

Iddi Ssessanga
19 Oktoba 2017

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amesema anaweza kutafakari upya uamuzi wake wa kujitoa kwenye uchaguzi mpya wa rais, iwapo kutakuwepo na hatua katika kuufanyia marekebisho mchakato wa uchaguzi.

Kenia Raila Odinga, Oppositionsführer | Interview in London, Großbritannien
Picha: Reuters/P. Nicholls

Odinga amayasema hayo baada ya kufanya mkutano na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Wafula Chebukati, ikiwa imesalia wiki moja tu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mpya wa rais, ambao umeitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro mkubwa wa kisiasa.

"Ikiwa mashauriano yatafanyika vizuri na ikiwa mageuzi sahihi yatafanyika, na hofu tulizozungumzia zikashughulikiwa, ambazo zilitufanya tujiondowe katika kinyanganyiro, basi tutafikiria upya.  Lakini kwa hali inavyoonekana sasa, msimamo wetu unabakia pale kama tulivyotangaza jana," alisema Odinga.

Siku ya Jumatano Odinga alihutubia mkutano uliohudhuriwa na maelfu ya wafuasi wake, na kuapa kwamba hakutakuwepo na uchaguzi, na kuongeza kuwa chama chake kitaitisha maandamano makubwa siku ya uchaguzi.

Odinga akihutubia wafuasi wake mjini Mombasa Oktoba 15,2017.Picha: Reuters/J. Okanga

Odinga bado kujitoa rasmi

Kiongozi huyo wa chama cha ODM alitangaza wiki iliopita kwamba hatoshiriki uchaguzi mpya wa rais kutokana na matatizo kwenye tume ya uchaguzi IEBC. Lakini alikuwa hajawasilisha barua rasmi ya kuondoa jina lake kwenye karatasi za kura, hatua ambayo inampa nguvu rais Kenyatta.

Amesema wasiwasi wao kuhusu IEBC umethibitishwa na matukio yaliotokea jana, katika taarifa za Chebukati na kamishna wa tume hiyo Roselyn Akombe, aliejiuzulu kuhusiana na madai ya machafuko ndani ya tume hiyo. Hayo yote yanatia kiwingu uwezekano wa kufanyika uchaguzi wa kuaminika.

Odinga amesema hivi sasa ni dhahiri kwa kila mtu kwamba mazingira ya sasa hayawezeshi kufanyika uchaguzi huru na wa haki. Siku ya Jumatano, Chebukati aliwasihi Odinga na Kenyatta kukutana naye ili kutuliza wasiwasi.

Kenyatta amburuza Odinga mahakamani

Lakini Rais Kenyatta amekataa kuahirisha uchaguzi na kusema mazungumzo yoyote yanapaswa kulenga kuhakikisha kuwa uchaguzi wa Alhamisi ijayo unafanyika vizuri na kwa amani. Na badala yake chama cha Kenyatta cha Jubilee kimefungua kesi ya kudharau mahakama dhidi ya Odinga na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka kuhusiana na wito wao wa kuwataka Wakenya wasusie uchaguzi huo.

Rais Uhuru Kenyatta amemburuza Odinga mahakamani kwa kuidharau mahakama.Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju amesema baada ya mahakama ya juu kuamuru uchaguzi mpya ndani ya siku 60 baada ya kufuta ushindi wa Rais Kenyatta, Odinga na Musyoka wamekuwa wakidharau maagizo ya mahakama hiyo. Amesema pia viongozi hao wa NASA na wafuasi wao wamezuwia mafunzo kwa maafisa wa uchaguzi katika ngome za Ondinga katika mkoa wa Nyanza.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Josephat Charo