ODM huko Kenya yageuza uongozi wake
27 Machi 2026
Kuna mpasuko kwenye chama hicho cha ODM hasa baada ya kambi ya Linda Mwananchi kujitenga na kuamua kufanya mkutano mwingine pembeni.
Kongamano hilo limefanyika kwa mara ya kwanza bila ya muasisi wake Raila Amolo Odinga.
Vurugu na demokrasia haviambatani
Kongamano hilo lililofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri liliwaleta pamoja wajumbe wapatao alfu tatu waliotumia fursa hiyo kuwapa ridhaa rasmi viongozi wa ODM walioteuliwa hivi karibuni.
Kiongozi wa chama Oburu Oginga alisisitiza kuwa demokrasia halisi haikumbatii vurugu.
"Bila madaraka huwezi kutimiza mipango ,sera na ahadi kwa wananchi. Kwahiyo madaraka kwanza mengine yatafwata,” alisema Oburu.
Mwenyekiti wa Orange Democratic Movement, ambaye pia ni gavana wa kaunti ya Homa Bay, Gladys Wanga aliwahimiza wajumbe kufuata maadili ya chama ili kuwa na sauti moja.
Ahmed Abdullahi alichaguliwa kuwa katibu mwenezi na naibu wake ni Mwakilishi wa wanawake bungeni katika kaunti ya Kisumu Ruth Odinga huku Otiende Amollo aliye pia mbunge wa Rarieda na mbunge wa Turkana South Ariko Nyamoit wamechaguliwa kuwa manaibu wenyekiti.
Yote hayo yakiendelea, kongamano hilo la kilele lilitumika pia kuwatimua baadhi ya wajumbe kwenye ngazi ya uongozi wanaosadikika kuwa waasi chamani.
Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi aliyesusia mkutano huo wa leo alivuliwa taji la kuwa mmoja wa manaibu viongozi watatu wa chama. Osotsi alikabidhiwa nafasi hiyo mwanzoni mwa Agosti mwaka 2024 pamoja na Gavana wa Kisii Simba Arati na mwenzake wa Mombasa Abdulswamad Nassir ambao bado wanashikilia nafasi hizo.
Vijana wapewe nafasi ODM
Katika tukio ambalo halikutarajiwa, Winnie Odinga ambaye ni mbunge wa bunge la Afrika Mashariki EALA aliyekuwa akiandamana na kambi ya Linda Mwananchi, alihudhuria kongamano la kilele na kuurai uongozi kuwapa vijana nafasi chamani.
”Nilisema juzi ODM ni nyumbani.Leo sikuja kuchoma,” alisema Winnie Odinga.
Kwa upande mwengine,purukushani zilizuka kwenye ukumbi wa Ufungamano ulikopangiwa mkutano wa kambi ya Linda Mwananchi.
Katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna aliye pia Seneta wa kaunti ya Nairobi naye pia alisusia kongamano la kilele na badala yake kuhudhuria kikao kilichoandaliwa ukumbini Ufungamano cha Linda Mwananchi.
Ifahamike kuwa Seneta Edwin Sifuna anavutana na uongozi wa ODM kwa kushikilia kuwa yeye ndiye katibu mkuu rasmi wa chama ilhali wahusika wakuu wamemtenga japo mahakama inashikilia kuwa ipo fursa ya kutatua mkwamo huo chamani.
Akiwa jukwaani Edwin Sifuna alikabiliana na purukushani kidogo na kulazimika kuwatolea maneno makali maafisa wa usalama.
"Huu ndio mkutano ambao tumendaa ili kuonyesha kuwa ODM iko katika hatyari kubwa sana.Wakora wameingia ODM.Tuliwaambia tunataka konamano la kitaifa ili kila mmoja aende debeni.Tunataka kura ya viongozi wa chama,” alisema Sifuna.
Maslahi ya umma ndio ajenda
Kambi ya Ufungamano ya Linda Mwananchi iliungwa mkono pia na Gavana wa Siaya James Orengo na mbunge wa Embakassi East Babu Owino.
Babu Owino alishikilia kuwa wanamheshimu Oburu Oginga kama kigogo wa siasa na wala sio kiongozi wa chama na kwamba maslahi ya umma ndio ajenda yao.
"Sisi ambao tuko hapa tutazidi kuwapigania, kwa sababu Mkenya anateseka."
Azma ya kongamano hilo la Kibra ni kutoa ridhaa rasmi kwa uongozi mpya, kujaza mapengo na kuandaa mkakati wa ODM kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao wa 2027.