Ofisi ya kazi ya Shirikisho ya Ujerumani yatoa takwimu juu ya ukosefu ajira
28 Februari 2006Kiwango cha wasio na kazi nchini Ujerumani katika mwezi uliopita kimepanda kutoka asili mia 12.1 hadi 12.2 katika mwezi huu wa februari, huku idadi ya waliorodheshwa kuwa hawana ajira ikiongezeka kwa 36,000 na kufikia milioni 5 na 48 elfu. Ofisi ya kazi ya Shirikisho pamoja na hayo inasema kwamba kiwango hicho kinachogonga vichwa vya habari katika taifa hili kubawa kiuchumi barani Ulaya, ni cha kawaida katika kipindi hiki cha baridi kali na hivyo ina matumaini hali itabadilika.
Mkuu wa ofisi hiyo Frank-Juergen Weise alisema idadi ya wasio na kazi imekua ikipungua kwa miezi kadhaa sasa. Hata hivyo takwimu tafauti zilizochapishwa na Benki ya Ujerumani Bundesbank zinaonyesha kupungua kwa ukosefu wa ajira kwa nafasi 5,000 na inasema idadi jumla ya wasio na kazi katika mwezi huu Februari ni milioni 4 na 695 elfu .
Upande wa magharibi idadi ya wasio na kazi ilipungua kwa kiwango cha 10,000 kufikia milioni 3 na 144 elfu na upande wa mashariki imepungua kwa 5,000 ikiwa sasa ni milioni 1 na 551 elfu. Pamoja na hayo Idadi hiyo kwa mwezi huu wa Februari ni bora kuliko ilivyokua mnamo mwezi kama huu mwaka uliopita, pale idadi ya wasio na kazi ilipogonga kiwango cha juu kuwahi kuonekana tangu vita vya pili vya dunia ilipofikia milioni 5 na 216 elfu, ikiwa ni asili mia 12.6
Mwana uchumi wa Deutschebank Stefan Bielmeier- anasema ukosefu wa kazi hakupanda mno na upungufu wa nafasi za kazi unaelekea kusita. Kuna matumaini ya kupatikana karibu nafasi 160,000 za kazi mnamo mwaka huu.
Taarifa ya Ofisi ya kazi ya Shirikisho inafuatia ile iliotolewa kabla na Benki kuu ya Ulaya juu kiwango cha ughali wa maisha nchini Ujerumani, ikisema kimesalia pale pale katika asili mia 2.1. Pamoja na hayo ni cha juu kuliko Februari mwaka jana. Hayo yametokana na takwimu za bei bidhaa kutoka mikoa muhimu kama Bavaria, Brandenburg, Hesse,North Rhine Westphalia na Saxony.
Takwimu hizi zimetolewa katika wakati ambao kesho serikali ya mseto ya vyama vikubwa vya kisiasa vya CDU/CSU na SPD ikitimiza siku 100 tangu kuingia madarakani chini ya Uongozi wa Kansela Angela Merkel, huku wadadisi na wataalamu wa uchumi wanasema bado kansela na serikali yake hawajafanikiwa kusawazisha matatizo ya kiuchumi yanayoikabili Ujerumani, licha ya kuidhinishwa mpango wa kupunguza nakisi kubwa katika matumizi ya serikali na kuanzisha mradi mkubwa wa kuvutia vitega uchumi.