Israel yakanusha Hamas kukubali pendekezo la kusitisha vita
15 Januari 2025Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, imekanusha kwamba kundi la Hamas limekubaliana na pendekezo lililoko mezani lililotolewa na wasuluhishi wa Qatar la usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza.
Ofisi ya Netanyahu imekanusha taarifa iliyotolewa na afisa wake mmoja aliyesema kundi la Hamas limeridhia pendekezo hilo. Ofisi ya Netanyahu inasema bado kundi la Hamas halijatowa jibu lake kuhusu mkataba huo.
Soma pia: Hamas yakubali rasimu ya makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka
Tangazo la Israel limetolewa leo wakati wasuluhishi nchini Qatar wamerudi tena mezani kwa mazungumzo yanayotarajiwa kupata mwafaka wa mwisho wa makubaliano ya usitishaji vita Gaza na kuachiliwa kwa wafungwa.
Jana maafisa wa Qatar, Misri na Marekani pamoja na Israel na Hamas walisema makubaliano ya usitishaji vita Gaza yanakaribia kufikiwa.