1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ofisi za usajili wa wagombea wa uchaguzi Kongo zafunguliwa

Jean Noel Ba-Mweze26 Juni 2023

Ofisi za kupokea na kushughulikia maombi ya wagombea kwenye uchaguzi wa Desemba katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, BRTC, sasa ziko wazi kwa wagombea ubunge wa kitaifa.

DR Kongo Kinshasa CENI Wahlkommission
Picha: Dirke Köpp/DW

Tume huru ya uchaguzi, CENI, hapo jana Jumapili imewaalika wagombea kuwasilisha maombi yao kuanzia leo Jumatatu. Tume hiyo lakini pia imetangaza kuahirisha hadi tarehe ambayo haijulikani, usajili wa wapiga kura katika eneo la Kwamouth mkoani Mai-Ndombe. Kwa maelezo kamili,

Ni ofisi 171 kwa ujumla ndizo zilizofunguliwa leo Jumatatu kwenye eneo lote la Kongo ili kupokea na kushughulikia maombi ya wagombea ubunge wa kitaifa. Ofisi hizo zitakuwa wazi kila siku kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi unusu jioni. 

Wagombea ambao hawakuweza kusajiliwa wakati zoezi hilo lilikuwa likifanyika miezi kadhaa iliyopita sasa watajisajili katika ofisi hizo hizo kabla ya kuwasilisha maombi yao. Ndivyo alivyoeleza Denis Kadima ambaye ni mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi, CENI, akibainisha pia kwamba wale ambao vyeti vyao vya uchaguzi tayari vimeharibika watapewa nakala katika ofisi hizo: "CENI inakumbusha kuwa muda wa kupokea na kushughulikia maombi ya ugombeaji wa wabunge wa kitaifa ni siku 20 tangu Juni 25 hadi Julai 15, na hivyo, inawaalika wagombea na vikundi vya kisiasa kuheshimu mpango huo. Uchaguzi ni mchakato unaohitaji ushiriki wa wadau wote. Chaguzi zote zinazofanyika kote ulimwenguni hutoa washindi na walioshindwa."

Mkuu wa tume ya uchaguzi Kongo Denis KadimaPicha: Facebook

Shughuli ya usajili wa wapiga kura katika eneo la Kwamouth mkoani Mai-Ndombe ilikuwa imepangwa kuanza leo Jumatatu. Lakini imeahirishwa kufuatia hali ya ukosefu wa usalama inayoendelea katika eneo hilo ambapo maelfu ya watu tayari wameuawa tangu ulipoanza mzozo baina ya jamii ya Wateke na Wayaka mwaka mmoja uliopita. Wakazi kadhaa wamekimbia vijiji vyao na hofu ni kwamba kuna dalili kuwa ukosefu wa amani unaweza ukaendelea huko kama serikali haitochukua hatua za haraka, kama alivyoonya Willy Bolio ambaye ni mbunge wa kitaifa kutoka eneo hilo.

"Tumefikia zaidi ya watu 2,000 waliouwawa na tuna watu kadhaa waliokimbia ambao ni vigumu kuwahesabu kwani hawako pamoja. Wahamiaji wetu wapo wengi hapa Kinshasa, wengi wapo mjini Bandundu na katika eneo la Bolobo. Wengine wengi sasa ni wakimbizi huko Kongo Brazzaville. Vikosi vya ulinzi wa usalama havifanyi chochote ila suluhu ni kwamba serikali lazima iamuru jeshi kuwaondoa hao wahalifu  wote."

Na huko mashariki mwa Kongo pia CENI haikuwasajili wapiga kura katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa waasi wa M23 mkoani Kivu Kaskazini kufuatia hali hiyo hiyo ya ukosefu wa usalama. Haya yanajiri huku Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ikiandaa kufanya chaguzi nne Desemba 20 zikiwemo uchaguzi wa rais, wa wabunge wa kitaifa na wa mikoa, pamoja na chaguzi za manispaa.