1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

OIC kupinga rasmi Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel

13 Desemba 2017

Rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmud Abbas amesema Wapalestina hawatakubali Marekani kuwa na jukumu lolote katika mchakato wa kutafuta amani kwenye mzozo wa Mashariki ya Kati kwa sababu inaipendelea Israel.

Türkei Sondergipfel der Organisation für Islamische Kooperation (OIC)
Picha: picture-alliance/AP Photo/L. Pitarakis

Rais huyo wa mamlaka ya ndani ya Palestina ameushutumu vikali uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel akisema uamuzi huo ni uhalifu mkubwa na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Kiongozi wa mamlaka ya Palestina Mahmoud AbbasPicha: picture-alliance/dpa/Str.

Akizungumza katika mkutano huo wa dharura wa nchi za Kiislamu ulioitishwa na Uturuki, Abbas amesisitiza Jerusalem imekuwa na itaendelea kuwa mji mkuu wa Palestina na kuongeza kusema Marekani imevuka mstari mwekundu kwa kuipa Israel mji wao kama ambao ni mji wa Marekani na kuapa hakutakuwa na amani wala uthabiti Mashariki ya Kati hadi pale Jerusalem itatambuliwa kuwa mji mkuu wa Palestina. Palestina imesema italiomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la kubatilisha uamuzi wa Trump,uamuzi ambao imesema unatishia dini zote.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Reuters/K. Ozer

Mwenyeji wa mkutano huo Rais Recep Tayyip Erdogan pia ameishutumu vikali Israel na kulitaja taifa hilo kuwa ni la kigaidi. Erdogan amesisitiza Jerusalem ndiyo mstari mwekundu kwa waislamu ambao hawatakubali uchokozi na ubabe katika maeneo yao matakatifu. Erdogan ameitaka jumuiya ya Kimataifa kutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Palestina akitilia mkazo suala la kuwa nchi za Kiisalmu hazitavunjika moyo katika azma yao ya kuhakikisha Palestina inatambuliwa kama taifa.

Viongozi na maafisa wa ngazi za juu kutoka nchi za ulimwengu wa kiislamu wanatarajiwa kufikia msimamo wa pamoja dhidi ya uamuzi wa rais wa Marekani Donald Trump wa kuutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel. Tangazo la Trump alilolitoa tarahe 6 mwezi huu wa Desemba kutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel limelaaaniwa vikali na nchi za Kiislamu na Jumuiya ya kimataifa. Kuna wasiwasi kuwa hatua hiyo ya Marekani itasababisha msukosuko zaidi Mashariki ya Kati na kuyapa nguvu makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali.

Kwenye mkutano wa awali  wa mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi wanachama wa jumuiya hiyo ya OIC uliofanyika mapema leo mjini Istanbul waziri wa mambo ya nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, alielezea kwamba Marekani inalenga kuhalalisha jitihada za Israel za kutaka kuuchukua kimabavu mji wa Jerusalem na mkutano huo mkuu lengo lake ni kuupinga udhalimu huo.

Mwandishi: Zainab Aziz

Mhariri: Caro Robi

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW