Olimpiki 2012 :Malkia azindua rasmi
28 Julai 2012Malkia Elizabeth alizindua rasmi michezo hii ya Olympiki jana usiku.Katika salam zake kwa wanamichezo na watazamaji Malkia Elizabeth alisema.
"Katika timu zetu zote za Olympiki kuna mambo mengi ambayo tunaweza kujivunia, makundi ya vijana wanaume na wanawake wenye shauku kubwa ya kufanya vizuri na kushinda michezo mbali mbali. Na timu hizi zinaungwa mkono kwa dhati na maelfu ya watayarishaji , watu wanaojitolea, na mashabiki, ambao watafuatilia mashindano haya, sio tu katika viwanja vya Olympiki hapa Uingereza lakini duniani kote. Kwa sababu hizi zote nawatakia nyie pamoja na nchi zenu mafanikio , na kuyafurahia mashindano haya ambayo mtayakumbuka wakati wote"
Michezo ya mbio za baiskeli na kuogelea ndio michezo mikubwa iliyoko katika mashindano ya Olimpiki hii leo Jumamosi (28.07.2012) mjini London wakati michezo hiyo ikiendelea baada kufunguliwa rasmi , katika sherehe kubwa na iliyofana sana ambayo imeelekezwa zaidi kwa kizazi kipya cha wanariadha. Bingwa wa dunia wa mbio za baiskeli Mark Cavendish atawania kuiletea Uingereza medali ya dhahabu katika mchezo huo.
Nae muogeleaji Michael Phelps amefanikiwa kukata tikiti ya kuingia fainali katika kuogelea kwa mchezaji mmoja mmoja katika fainali itakayofanyika jioni .
Michezo ya kulenga shabaha, mpira wa badminton, mpira wa meza na judo vilifanyika mapema asubuhi. Lakini sehemu kubwa ya Uingereza imeachwa na butwaa baada ya sherehe za ufunguzi hapo jana ambapo sherehe hizo ziliendelea hadi majira ya alfajiri hii leo.
Na huko mjini Dar Es Salaam timu za Yanga na Azam zote za mjini Dar Es Slaam zimefamefanikiwa kuingia fainali ya kombe la Kagame la vilabu bingwa katika Afrika mashariki na kati.
Mchambuzi wetu wa masuala ya soka nchini Tanzania Master Tindwa, amesema kuwa timu changa ya Azam , ambayo imeingia fainali katika mashindano makubwa kama haya kwa mara ya kwanza miaka mitano tangu kucheza katika ligi kuu ya Tanzania inatabiriwa kuwa nguvu mpya ya ushawishi wa soka nchini Tanzania na Afrika mashariki na kati kutokana na mapinduzi makubwa inayofanya katika soka katika ukanda huo.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe /rtre
Mhariri : Mohamed Dahman