Olimpiki: Michezo ya Sochi yafunguliwa rasmi
8 Februari 2014Rais Putin amelenga kutuliza hofu za mashambulizi ya kijeshi na pia kuondoa mzozo kuhusiana na haki za mashoga , hali iliyotia doa wakati mashindano hayo yanakaribia kuanza.
Putin ameimarisha hadhi yake kwa nchi yake kuwa mwenyeji wa mashindano salama na ya mafanikio ya olimpiki katika mji wa kitalii katika bahari nyeusi wa Sochi, ambako tamasha la ufunguzi lililokuwa na kila aina ya shamra shamra katika uwanja uliosheheni watazamaji 40,000 katika uwanja mpya wa Fisht uliashiria mwanzo wa mashindano hayo kwa ukamilifu.
"Natangaza mashindano haya ya 22 kuwa yamefunguliwa" amesema Putin akifungua rasmi tukio hilo ambalo anatarajia kuwa litasafisha heba yake pamoja na nchi yake duniani. Rais wa kamati ya kimataifa ya olimpiki Thomas Bach amesema haya yatakuwa mashindano ya kuvutia.
"Kuna hamasa kubwa na nina matarajio mwenge wa olimpiki ukiwaka katika uwanja wa olimpiki, hata wanamichezo watakuwa katika hali kama hiyo na nina hakika litakuwa tamasha la kufurahisha."
Gharama za mashindano
Watayarishaji wametetea gharama za kuendesha mashindano hayo ya Sochi huku kukiwa na wasi wasi kutoka kwa maafisa wa olimpiki kuwa gharama kubwa huenda ikawaweka wadhamini kando katika mashindano yajayo.
Licha ya manung'uniko ya hapa na pale kuhusu maeneo ya malazi ambayo hayakukamilika katika sehemu kadha , hali miongoni wa washiriki wa mashindano hayo pamoja na maafisa wao baada ya michezo kadha ya mwanzo mjini Sochi imekuwa ya matumaini.
Michezo hiyo inaanza rasmi leo kwa wanamichezo kushindana katika michezo mbali mbali.
Bundesliga
Na katika kandanda, ligi ya Bundesliga imeingia katika mchezo wake wa 20 jana Ijumaa wakati Bayer Leverkusen ilifanikiwa kushinda mchezo wa kwanza kwa bao 1-0 dhidi ya Borussia Moenchengladbach na kuendeleza vipigo dhidi ya timu hiyo iliyokuwa ikicheza nyumbani.
Katika mchezo huo ambao haukuwa na mvuto wa kutosha na nafasi chache za kufunga Son Heung Min alidhihirisha kuwa ni mmoja kati ya wachezaji ambao wanaweza kubadili matokeo na kupachika bao pekee usiku huo katika dakika ya 62 ya mchezo.
Leo VFL Wolfsburg inaikaribisha Mainz , wakati Bremen inakibarua na Borussia Dortmund. Pambanoi la watani wa jadi linafanyika huko mkoani Bavaria ambapo Nürnberg inatiana kifuani na miamba wa Bundesliga Bayern Munich.
Alipoulizwa kuhusu pambano hilo kocha wa Bayern Pep Guardiola amesema lolote linaweza kutokea, kwani pambano la watani wa jadi mara zote halitabiriki. Lakini amesisitiza kuwa kikosi chake kinataka kuhakikisha kuwa hakipotezi mchezo.
Freiburg inamiadi na Hoffenheim , Eintracht Frankfurt inaikaribisha Eintracht Braunschweig , wakati Hamburg itaoneshana kazi na Hertha BSC Berlin.
Kesho Jumapili (09.02.2014) ni zamu ya Stuttgart kuoneshana kazi na Augsburg na Schalke wanaikaribisha Hannover nyumbani.
Huko Uingereza Aston Villa ina miadi na West Ham United, Chelsea iko nyumbani ikiisubiri Newcastle, Crystal Palace inapimana nguvu na West Bromwich Albion , na pambano la kukata na shoka jioni ya leo ni kati ya mafahali wawili Liverpool ikiwa nyumbani inaikaribisha Arsenal London ambayo ni kinara wa ligi hiyo kwa sasa.
Insert
Mwandishi: Sekione Kitojo
Mhariri:Yusuf Saumu