1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Olimpiki Paris 2024: Wanariadha wa Afrika wang´ara

3 Agosti 2024

Wanariadha kutoka nchi za Kiafrika wamepata fursa ya kuonyesha uwezo wao wakati wakishiriki mashindano hayo huku China ikiendelea kuongoza katika jedwali la medali.

Joshua Cheptegei mwanariadha wa Uganda
Mwanariadha raia wa Uganda Joshua Cheptegei, aliyeshinda katika mbio za mita 10,000 kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris mwaka 2024.Picha: Petr David Josek/AP

Miongoni mwa wanariadha kutoka nchi za Kiafrika waliopata fursa ya kuonyesha uwezo wao hapo jana ni pamoja na raia wa Uganda Joshua Cheptegei, aliyeshinda ubingwa wa Olimpiki katika mbio za mita 10,000 kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris mwaka 2024.

Cheptegei mwenye umri wa miaka 27 na ambaye ni bingwa wa dunia mara tatu na mshindi wa medali ya fedha ya  Olimpiki mjini Tokyo mwaka  2021, alishinda taji lake la pili la Olimpiki, miaka mitatu baada ya mbio za mita 5,000 mjini Tokyo.

Mwanariadha huyo wa Uganda alishinda baada ya dakika 26 na sekunde 43 ikiwa ni rekodi mpya ya Olimpiki, na kuwapiku Muethiopia Berihu Aregawi na Mmarekani Grant Fisher.

Mashindano ya soka ya wanaume na kuogelea

Misri ilifanikiwa jana Ijumaa kufuzu katika hatua ya nusu fainali kwa kuifunga Paraguay kwa mikwaju ya penalti, katika mechi iliyochezwa mjini Marseille.

Katika mechi ya nusu fainali siku ya Jumatatu mjini Lyon, Misri itamenyana na Ufaransa iliyoicharaza Argentina bao 1-0. Nusu fainali nyingine itazikutanisha Morocco na Uhispania siku ya Jumatatu huko Marseille.

Olimpiki-Paris 2024: Mwogeleaji raia wa Marekani Caeleb DresselPicha: Gian Mattia D'Alberto/LaPresse via ZUMA Press/picture alliance

Ama katika michuano mingine, shujaa wa Michezo hii ya Olimpiki ya Paris, mwogeleaji raia wa Ufaransa Léon Marchand alishinda medali yake ya nne ya dhahabu jana Ijumaa katika mchuano wa kuogelea mita 200 na hivyo kukamilisha wiki iliyokuwa na manufaa makubwa kwa mwanamichezo huyo mwenye umri wa miaka 22 ambaye hajawahi kutokea katika historia ya mchezo wa kuogelea nchini Ufaransa.

Soma pia: Michuano ya Michezo ya Olimpiki Paris 2024 yaendelea

Bingwa wa dunia mwaka wa 2023, Muaustralia Cameron McEvoy alipata ubingwa wa Olimpiki baada ya kuogelea mita 50 ndani ya muda wa dakika 21 na sekunde 25. McEvoy aliwashinda Briton Benjamin Proud na Mfaransa Florent Manaudou.

Akiwa na umri wa miaka 30, McEvoy alishinda jana taji lake la kwanza la Olimpiki baada ya medali mbili za shaba mjini Rio na nyingine ya tatu mjini Tokyo.

Katika michuano ya mpira wa kikapu

Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020: Mechi kati ya Ujerumani na NigeriaPicha: Charlie Niebergall/Pool/REUTERS

Katika michuano ya Handball upande wa wanaume, Ujerumani, Slovenia na Misri zilifuzu jana na kuingia robo-fainali huku nafasi tatu za mwisho zitarajiwa kugombaniwa kesho Jumapili.

Ujerumani iling´aa katika michuano hiyo hapo jana, ambapo katika mchezo wa mpira wa kikapu, iliicharaza Ufaransa 85-71 wakati wa mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi kwenye Uwanja wa Pierre-Mauroy huko Villeneuve-d'Ascq.

Soma pia: Michezo ya Olimpiki Paris 2024: China yaongoza kwa medali za dhahabu

Ufaransa ambao walikuwa tayari wamefuzu katika hatua ya robo fainali hata kabla ya mechi hiyo, walimaliza katika nafasi ya pili katika kundi B, nyuma ya Ujerumani ambao walithibitisha ubingwa wao katika kuwania medali ya Olimpiki.

Katika jedwali la medali, China bado iko kileleni na jumla ya medali 13 za dhahabu, ikifuatiwa mara hii na Ufaransa yenye 11, Australia ikishika nafasi ya tatu na medali 11 na Marekani nafasi ya nne. Ujerumani bado iko nafasi ya 11 na medali mbili tu za dhahabu.

(Vyanzo: Mashirika)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW