1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Oman yaendeleza upatanishi Wahouthi, Saudi Arabia, Iran

9 Aprili 2023

Saudi Arabia imewaachia huru wafungwa kadhaa wa kivita wa kundi la Wahouthi nchini Yemen, huku wapatanishi wa Oman wakiwasili mjini Sanaa katika juhudi za kukomesha mgogoro wa miaka mingi nchini Yemen.

EINSCHRÄNKUNG Oman | Robert Malley, Sondergesandter für den Iran der Vereinigten Staaten
Picha: Tasnim

Abdul-Qader el-Murtaza, afisa wa waasi wa Kihouthi anayehusika na mazungumzo ya kubadilishana wafungwa, alisema siku ya Jumapili (Aprili 9) kwamba wafungwa wao 13 waliwasili siku ya Jumamosi kwenye mji mkuu wa Yemen, Sanaa.

Alisema wafungwa hao waliachiliwa kwa mabadilishano na mfungwa mmoja wa Kisaudi aliyekuwa ameachiliwa kabla na Wahouthi. Hakusema ni wakati gani waasi hao walimuachia huru mfunngwa huyo wa Kisaudi.

Soma zaidi: Saudi Arabia na Wahouthi watafuta suluhu Yemen

Mabadilishano hayo ya wafungwa ni sehemu ya mpango unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa ambao uliafikiwa na pande hasimu kwenye vita vya Yemen na unaojumuisha kuachiliwa huru wafungwa wapatao 900 kutoka pande zote mbili, alisema el-Murtaza.

Mpango huo wa Umoja wa Mataifa umepangiwa kuanza kutekelezwa mwezi huu. 

Oman yatuma ujumbe wa upatanishi

Wakati huo huo, maafisa wa timu ya upatanishi kutoka Oman waliwasili mjini Sanaa kwa mazungumzo na maafisa wa Kihouthi siku ya Jumapili, wakiwa kwenye mojawapo ya juhudi za hivi karibuni kabisa kimataifa kurejesha makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yalimalizika muda wake mwezi Oktoba.

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Martin Griffiths.Picha: Fabrice Coffrini/AFP

Kwa miaka mingi, Oman imekuwa mwenyeji wa mazungumzo kati ya waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran na Saudi Arabia inayoongoza muungano wa kijeshi dhidi yao. Mazungumzo hayo yamezidi kuwa ya kina tangu pande hizo hasimu kushindwa kuongeza muda wa kusitisha mapigano ulipomalizika.

Soma zaidi: Hofu ya vita yarejea Yemen kwa kushindwa kurefusha mkataba

Kituo cha televisheni cha al-Masirah kinachoendeshwa na Wahouthi kiliripoti kwamba ujumbe wa Saudi Arabia ukiongozwa na balozi wa nchi hiyo nchini Yemen, Mohammed bin Saeed Al-Jaber, nao pia ungeliwasili siku ya Jumapili kwa mazungumzo na Wahouthi.

Mazungumzo yaliyokuwa yakifanyika kwenye mji mkuu wa Oman, Maskati, yalijikita kwenye kuzuia kuzuka kwa vita vyengine vikubwa baada ya kuvunjika kwa usitishaji mapigano, na kuweka njia ya kufikiwa makubaliano ya kukomesha vita moja kwa moja nchini Yemen.

Mazungumzo hayo yamezidi kupata nguvu katika wiki za hivi karibuni baada ya Saudi Arabia kufikia makubaliano na Iran juu ya kurejesha mahusiano yao ya kidiplomasia kufuatia miaka saba ya mzozo baina yao.

Soma zaidi: Yemen: Watu 53 wauawa katika mapigano kuwania mji wa Marib

Makubaliano hayo yaliyotangazwa mjini Beijing, China, tarehe 10 Machi, yameibua matumaini ya kuumaliza moja kwa moja mzozo wa vita nchini Yemen.

Sehemu ya Chuo Kikuu cha Aden ilivyoharibiwa na mashambulizi ya angani.Picha: Saleh Al-Obeidi/AFP/Getty Images

Ulikoanzia mzozo wa Yemen

Vita vilianza nchini Yemen mwaka 2014, baada ya Wahouthi kutwaa udhibiti wa mji mkuu, Sanaa, na sehemu kubwa ya kaskazini mwa nchi hiyo ya kusini mwa Uarabuni, kwa kuiondowa serikali inayotambuliwa kimataifa ambayo ilikimbia upande wa kusini na baadaye uhamishoni nchini Saudi Arabia.

Soma zaidi: Oman yasema muafaka wa Yemen upo njiani

Miezi kadhaa baadaye, muungano wa kijeshi unaongozwa na Saudi Arabia ulijiingiza kwenye mzozo huo kwa nia ya kuirejesha madarakani serikali hiyo inayotambuliwa kimataifa, na tangu hapo mzozo huo umegeuka vita vya kikanda baina ya mahasimu wakubwa, Saudi Arabia na Iran, kila mmoja akiunga mkono upande mwengine.

Zaidi ya watu 150,000, wakiwemo raia na wapiganaji, wameshauwa kwenye vita ambavyo vimesababisha mojawapo ya majanga makubwa kabisa ya kibinaadamu duniani. 

Vyanzo: AFP/DPA