1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Omanyala hatoshiriki mashindano ya riadha ya dunia Marekani

14 Julai 2022

Mwanariadha mwenye kasi zaidi barani Afrika Ferdinand Omanyala amesema atakosa kushiriki mashindano ya riadha ya dunia yanayofanyika nchini Marekani kwa sababu ya kucheleweshwa kupata cheti cha kusafiri nchini humo.

Leichtathletik | Afrikameisterschaft Mauritius 2022
Picha: Deji Ogeyingbo

Mwanariadha huyo Mkenya aliye na umri wa miaka 26 Ferdinand Omanyala, alikuwa na matumaini ya kufanya vizuri kabisa katika mbio za mita 100 kwenye mashindano hayo ya riadha ya dunia yatakayoanza rasmi Ijumaa (15.07.2022) mjini Eugene katika jimbo la Oregon Marekani lakini hilo kwa sasa haliwezekani.

"Nimekata tamaa na kuachana na safari yangu ya Oregon maana hata nikipata Visa leo tayari nimechelewa, sipendi kungoja na nimesubiri sana, hata nikikata tiketi leo, siwezi kufika kwa wakati kushiriki mashindayo hayo, haiwezekani hata kidogo," alisema Omanyala alipozungumza na shirika la habari la AFP. 

Mwanariadha huyo alitarajiwa kushiriki katika mashindano ya mbio hizo hapo kesho lakini kwa sasa hatoweza kusafiri kufuatia Viza yake kutolewa kuchelewa na hawezi kushiriki kutokana na safari yenyewe kuchukua masaa 24 na zaidi hadi jimboni Oregon.

Timu ya Kenya ilipaswa kuondoka kuelekea Marekani siku ya Jumatatu na Jumanne na Omanyala alikuwa miongoni mwa wanariadha ambao hawakuwa wamepata Viza zao hadi wakati huo. Hadi sasa hapajatolewa maoni yoyote kutoka kwa shirika la Riadha la Kenya juu ya hili na sababu za kumcheleweshea Viza yake pia bado hazijajulikana.

Hata hivyo kuna ripoti zilizoibuka za wanaridha wengine kutoka mataifa mengine waliopata matatizo ya kupata vyeti vyao vya kusafiria. Waandaaji wa mashindano ya Oregon22 na mashindano ya riadha ya dunia wamesema wanafuatilia kujua sababu ya kucheleweshwa kutolewa Viza kwa baadhi ya wanariadha lakini wakasema kuwa usafiri wa kimataifa umekuwa na changamoto nyingi kutokana na janga la virusi vya corona.

Omanyala alitarajia kuweka rekodi mpya katika mashindano ya Oregon22

Mwanaridha wa Kenya Ferdinand Omanyala akiwa na mwenzake wa Afrika Kusini Akani Simbine katika mashindano ya riadha ya Afrika yalioyofanyika Mauritius Picha: Deji Ogeyingbo

Ferdinand Omanyala ndiye mtu wa tatu mwenye kasi zaidi duniani akiwa nyuma ya Wamarekani Fred Kerley na Trayvon Bromell kwa kuweka rekodi ya sekunde 9.85 mwezi Mei. Septemba mwaka jana alivunja rekodi katika mashindano ya riadha ya Afrika kwa kukimbia kwa sekunde 9.77 na kumuweka katika nafasi ya 9 ya watu walio na kasi kubwa duniani akiwatupa nyuma wamarekani wanne na wajamaica watatu.

Omayala aliliambia shirika la habari la AFP kwamba katika mbio za mita 100 za Oregon alikuwa amejiwekea rekodi mpya ya kukimbia kwa sekunde 9.6. Angepata nafasi hiyo basi angeweka historia ya kuwa mwanariadha wa Afrika kuweka rekodi kama hiyo.

Omanyala amesema kwa sasa nguvu zake zote ameziweka katika mashindano ya Jumuiya ya Madola yatakayofanyika mjini Birmingham Uingereza kuanzia tarehe 28 Julai hadi tarehe 8 Agosti. Amesema kwa sasa atabakia tu kuwa mtazamaji katika mashindano ya Oregon22 huko Marekani.

Chanzo: afp

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW