Ombi la Ujerumani la kuachiwa Badawi lagonga ukuta
8 Machi 2015Gabriel ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha Social Demokratik nchini Ujerumani (SPD) amekaririwa akisema baada ya kukutana na mfalme huyo wa Saudi Arabia kwamba "Kila tunachokifanya kinamsaidia mwanabalogi huyo lakini hakuna mtu hata familia yake anayefikiri kwamba kutakuwa na ufumbuzi wa haraka kwa kisa hicho."
Badawi alihukumiwa mwaka jana kuchapwa viboko 1,000 na kutumikia kifungo cha miaka 10 gerezani kwa madai ya kuutukana Uislamu. Alichapwa viboko vya kwanza hamsini hadharani katika uwanja mmoja kwenye mji wa mwambao wa Jeddah hapo mwezi wa Januari lakini serikali ikasitisha kuendelea kuchapwa viboko hivyo baada ya kushutumiwa na mashirika ya haki za binaadamu na washirika wa mataifa ya magharibi wa nchi hiyo ya kifalme ikiwemo Marekani ilioitaka serikali ya Saudi Arabia ibatilishe hukumu hiyo na wizara ya mambo ya nje ya Sweden iliomwita balozi wa Saudi nchini mwao kupinga adhabu hiyo.
Adhabu ya viboko yaharibu taswira ya Saudia
Waziri wa uchumi wa Ujerumani Gabriel amesema kwamba amemueleza mfalme wa Saudia kwamba adhabu hiyo kali ya viboko imeharibu taswira ya Saudi Arabia nchini Ujerumani na kwamba ametaja uwezekano wa kumpatia msamaha Badawi.
Wakati wa mazungumzo yake ya masaa mawili na mfalme, Gabriel pia ametowa wito wa kuachiliwa kwa wakili wa Badawi ambaye naye amehukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani.
Wakili wake huyo Waleed Abul-Khair ambaye ni mtetezi mashuhuri wa haki za binaadamu amehukumiwa kifungo hicho kwa kuitukana mahakama miongoni mwa mashtaka mengine yanayohusiana na harakati zake za kisiasa.
Muda mfupi kabla ya kukutana na Mfalme wa Saudia, Gabriel aliokosowa amri ya mahakama ya kumuadhibu Badawi hususan ile ya kuchapwa viboko ambayo amesema ni jambo ambalo haliingii akilini kwa Wajerumani na bila ya shaka linauweka uhusiano kati ya nchi hizo mbili mashakani.
Wanaharakati wadai kuachiwa kwa Badawi
Kundi la wanaharakati nchini Ujerumani la Avaaz liliandaa maandamano mbele ya uwanja wa ndege wa Tegel ulioko Berlin kabla ya kuondoka kwa Gabriel hapo Jumamosi kuelekea katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh.
Waandamanaji hao walimkabidhi Gabriel ombi lenye saini za watu mbali mbali kusaidia kuachiliwa huru kwa Badawi na baruwa kutoka kwa mke wa Badawi ambaye anaishi Canada na watoto wake watatu.
Gabriel amewaambia waandishi wa habari kwamba serikali ya Ujerumani kwa wiki kadhaa imekuwa ikienda mbio kutaka kuachiliwa huru kwa Badawi.
Mashirika ya haki za binaadamu yanasema kesi dhidi ya Badawi ni sehemu ya ukandamizaji mkubwa wa uhuru wa kutowa maoni na upinzani nchini Saudi Arabia tokea Uasi wa Majira ya Machipuko ya Ulimwengu wa Kiarabu mwaka 2011.Kushutumiwa kwa masheik kunaonekana ni kufurutu ada kwa sababu ya hadhi waliyonayo katika nchi hiyo ya kifalme halikadhalika dhima yao yenye ushawishi katika kusaidia sera za serikali.
Serikali ya Saudia yashangazwa
Saudi Arabia imetowa kauli yake ya kwanza rasmi juu ya kesi hiyo hapo Jumamosi kwa kusema kwamba inaelezea mshangao wake mkubwa na kufadhaishwa kwa jinsi vyombo vya habari vya kimataifa vinavyoitangaza kesi hiyo.
Taarifa hiyo iliyotolewa na afisa wa wizara ya mambo ya nje ambaye hakutajwa jina na ambaye matamshi yake yametolewa na Shirika la Habari la Saudia akisema kwamba ufalme wa Saudi Arabia "haukubali kuingiliwa kati kwa aina yoyote ile katika masuala yake ya ndani ya nchi" na kwamba vyombo vyake vya mahakama viko huru na havina upendeleo. Taarifa hiyo imeongeza kusema kwamba katiba ya nchi hiyo ilioko chini ya misingi ya sheri ya Kiislamu inahakikisha kuheshimiwa kwa haki za binaadamu.
Awali Jumapili Gabriel alikutana na wanaharakati watatu wa kike kwa kwenda sambamba na Siku ya Wanawake Duniani.Gabriel anaongoza ujumbe wa watu 80 viongozi wa kibishara wa Ujerumani katika ziara yake hiyo ya nchi za Ghuba inayojumuisha pia Umoja wa Falme za Kiarabu na Qatar.
Mwandishi : Mohamed Dahman/ AP/dpa
Mhariri : Amina Abubakar