Ongezeko la vimbunga kanda ya Sahara
27 Aprili 2017Kanda ya jangwa la Sahel barani Afrika imeshuhudia ongezeko la mara tatu la vimbunga vya mvua vinanoleta taabu na uharibifu mkubwa badala ya kuleta manufaa tangu 1982. Hayo ni kwa mujibu wa utafiti juu ya mabadiliko ya tabia nchi uliotangazwa hapo siku ya Jumatano 26.04.2017. Wataalamu waliofanya utafiti huo wamesema iwapo hali ya kuongezeka kwa joto duniani haitatafutiwa ufumbuzi basi maeneo mengi katika kanda ya jangwa la Sahel yatakabiliwa na mvua kubwa kupita kiasi na mara kwa mara maeneo hayo yatakumbwa na mafuriko. Christopher Taylor mtaalamu wa maswala ya hali ya hewa amesema nchi ambazo zina upungufu wa miundombinu hazitaweza kupambana na athari hiyo. Taylor na timu yake walifanya uchunguzi wa mawingu kwa kutumia mitambo ya satellite mnamo mwaka wa1982-2016 ambapo walifuatilia mageuzi ya ruwaza ya dhoruba katika eneo la kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwa ni pamoja maeneo ya, Mauritania, Mali, Burkina Faso, Niger, Nigeria, Chad, Sudan na Senegal.