Uganda yashuhudia ongezeko la wafungwa wanawake
18 Novemba 2025
Kulingana na takwimu za mamlaka ya magereza, kati ya wafungwa 3,851 wanawake ambao wanatumikia kifungo baada ya kuhukumiwa ni 1,891.
Idadi nyingine iko rumande wakisubiri kesi dhidi yao kuamuliwa au kutokana na wadai wao kuwaweka gerezani hadi walipe deni.
Wanawake wengi hujikuta wamevunja sheria au kuhusika katika uhalifu na maovu ambayo vyanzo vyake ni hali ya mahusiano na wapenzi wao na kwa jumla mizozo na ukatili katika familia.
Hii huishia katika mauaji, majeraha kwa kupigana au hila zingine kuhusiana na ugomvi unaoibuka katika familia.
Masuala ya umiliki ardhi, mavuno shambani au mali yanaelezewa kuchochea mabishano kati ya mume na mke na kuishia katika uhalifu na maovu kama vile mauaji.
Umasikini unachangia wanawake wengi kutiwa hatiani
Lakini kwa mtazamo wa baadhi ya watu na pia uchunguzi ambao umefanywa na mamlaka ya magereza Uganda, umasikini na kutelekezwa kwa wanawake ni hali ambayo huwafanya wengi kujikuta katika makosa ya kuua, kupiga na kujeruhi na pia kuwasababisha watoto kuvunjiwa haki zao.
Kutokana na hali hiyo wanashauri kuwa familia iwe chanzo cha kujenga maridhiano na kutoa nasaha kwa wapendanao, wanandoa na hata jamaa zao kuhusishwa.
Zaidi ya nusu ya idadi ya wanawake magerezani wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji, kuua bila kukusudia au kujeruhi watu.
Asili mia 76 ya wanawake wafungwa huelezea kuwa wanatoka katika familia masikini huku asili mia 32 wakielezea kuwa hawakuapata fursa ya elimu shuleni. Wanajamii wanasema.
Wanawake na jukumu la familia
Suala la watu kufungwa na wadai wao huwahusu hata wanaume lakini kwa upande wa wanawake, watu wengi wana mtazamo kuwa si busara kuwafunga wanawake kutokana na madeni kwani wana majukumu ya kutunza familia zao hususan ikijulikana kwamba hali hiyo hutokana na jaribio la mwanamke kutaka kuwa na mtaji wa kuendesha biashara na njia rahisi ni kuchukua mkopo.
Lakini mambo huwaendea mrama kinyume na matarajio yao. Msemaji wa magereza Frank Baine ana mtazamo kwamba pana haja sheria ichunguzwe upya kuhusiana na suala hilo.
Isitoshe, kuna wanawake ambao hufungwa gerezani na watoto wao kwa sababu hawana mtu wa kuwatunza ila wao.
Hali hii inaelezewa kuwasababishia watoto wao kukosa fursa ya kuishi katika mazingira stahiki kwa makuzi yao.