1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watakaosababisha vurugu wakati wa uchaguzi waonywa Uganda

8 Januari 2021

Maafisa wa ngazi za juu wa vyombo vya usalama nchini Uganda wametoa onyo kali kwa yeyote ambaye ana nia ya kusababisha rabsha na vurugu katika uchaguzi utakaofanyika Alhamisi ijayo kwamba atajuta kuzaliwa.

Uganda Bobi Wine
Picha: Ronald Kabuubi/AP Photo/picture alliance

Tamko hilo la mkuu wa jeshi la polisi Uganda Michael OKoth Ochola linadhihirisha kuwa vyombo vya usalama vimejiandaa vilivyo kukabiliana na hali zozote zinakazoelekea kutatiza mchakato wa uchaguzi mkuu.

Lakini kwa upande mwingine limeelezewa na watu mbalimbali kuwatishia usalama wao wakitaja hali ya kampeni ambapo majeshi na polisi wameonekana waziwazi wakiwahujumu raia wasio na silaha.

Ikimbukwe kuwa watu 55 walipoteza maisha yao, 32 kati yao kutokana na risasi katika machafuko ya mwezi Novemba kufuatia kukamatwa kwa mgombea urais Robert Kyagulanyi.

soma zaidi:Uganda: Upinzani wazindua jukwaa la kufuatilia uchaguzi

Polisi imesisitiza kuwa watahakikisha kuwa agizo la tume ya uchaguzi wapiga kura wasibaki kwenye vituo baada ya kupiga kura linazingatiwa.

Waandishi habari oia wapo matatani Uganda

Picha: DW/Ole Tangen

Mkuu wa polisi Okoth Ochola pamoja na mawaziri wa usalama na wakuu wa magereza na makamanada wa jeshi wamewahutubia wanahabari leo kwenye makao makuu ya polisi. Amewaonya wanahabari kwamba wasitarajie kwamba polisi haitawashambulia pia kwani ina sababu zake inapofanya hivyo.

Wiki mbili zilizopita wanahabari walisusia kikao cha vyombo vya usalama kwenye kituo cha serikali za kueneza habari wakipinga vitendo vya vyombo vya usalama kuwaandama wanapofanya kazi yao. Walipotaka wakuu hao kuomba radhi kwa jumuiya hiyo walikataa.

soma zaidi: Wanaharakati wa haki za binaadamu wahofia usalama wao Uganda

Mwanahabari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa Ken Lukwago ameelezea tamko la mkuu wa polisi kudhihisha kuwa mateso na manyanyaso yanayofanywa dhidi ya wanahabari na majeshi na polisi kumbe ni agizo kutoka kwa wakuu wao.

Hadi sasa wanahabari 12 wamehujumiwa wakiendesha kazi zao na vyombo vya usalama katika kampeni zinazoendelea. Wanahabari wa kigeni ambao wamefanikiwa kupata ruhusa kufuatilia uchaguzi wamewekewa masharti makali huku wengine wengi wakinyima idhini ya kuja Uganda.

Mwandishi: Lubega Emmanuel/DW Kampala