1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Hofu ya mashambulizi yaongezeka katika hospitali Gaza

Angela Mdungu
30 Oktoba 2023

Wasiwasi umewagubika wakazi wa Gaza wanaojihifadhi katika hospitali kubwa zilizo kwenye ukanda huo baada ya Israel kutangaza uwezekano wa kufanya mashambulizi kwenye maeneo hayo.

Moshi ukifuka baada ya mashambulizi ya anga ya Israel katika Ukanda wa Gaza
Moshi ukifuka baada ya mashambulizi ya anga ya Israel katika Ukanda wa GazaPicha: Yasser Qudih/REUTERS

Baada ya Jeshi la Israel kuwataka watu waliojihifadhi kwenye hospitali ya Al Quds na katika kitongoji cha Ta al- Hawa waondoke kwenye maeneo hayo, wakaazi hao wameelezea wasiwasi wao huku wakisema kuwa hawana pa kwenda. Hata hivyo watu hao wamekataa kuondoka na kusalia hospitalini hapo. Kulingana na wizara ya mambo ya ndani na shirika la hilali nyekundu kwenye Ukanda wa Gaza zilisema kuwa tayari Israel imeshafanya shambulio lililosababisha uharibifu katika maeneo jirani na hospitali hiyo.

Nalo Jeshi la Israeli limesema vikosi vyake vimewauwa makumi ya "magaidi" ambao walijificha katika majengo na mahandaki na kujaribu kuwashambulia wanajeshi wake ndani ya saa 24 zilizopita. Katika moja ya mashambulizi hayo, ndege ya kijeshi ya Israel ililenga jengo lililokuwa na zaidi ya wapiganaji 20 wa Hamas ndani yake. Katika tukio jingine ndege  nyingine ilishambulia mfumo wa kuzuia makombora katika eneo la Chuo Kikuu cha Al-Ahzar katikati mwa mji wa Gaza.

Soma zaidi: Israel yaendeleza mashambulia yake Gaza

Eneo hilo limekuwa kitovu cha mashambulizi ya Israel tangu shambulio la Hamas la Oktoba 7. Jeshi hilo limesema lililenga zaidi ya maeneo 600 ya magaidi  yakiwemo maghala ya silaha, na maeneo iliko mifumo ya kuzuia makombora bila kusahau maficho na maeneo yanayotumiwa na Hamas katika siku za hivi karibuni.

Vikosi vya Israel vikijipanga karibu na mpaka wa GazaPicha: Ohad Zwigenberg/AP Photo/picture alliance

Kwa upande wao wapiganaji wa kundi la Hamas wameripoti pia mapigano makali katika eneo hilo ikiwa ni usiku wa tatu tangu Israel ilipotanua operesheni yake ya kijeshi kwa kutumia vifaru na magari ya kivita ndani ya ardhi ya Gaza iliyoharibiwa vibayakwa mashambulizi.

Idadi ya waliokufa yafikia watu 8,000

Kulingana na wizara ya afya ya Gaza iliyo chini ya kundi la Hamas, zaidi ya watu 8,000 wengi wao wakiwa ni raia wa kawaida wameuwawa tangu Israel ilipoanzisha operesheni ya kijeshi ya anga na ya ardhini. Wizara hiyo ya afya imeripoti pia kuwa watu wa nne wameuwawa mjini Jenin katika eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel la Ukingo wa Magharibi wakati majeshi ya Israelyalipokabiliana na Wapalestina.

Hayo yakiendelea, Umoja wa Mataifa umesema malori 117 yaliyobeba misaada yameingia Gaza tangu vita vilipoanza zaidi ya wiki tatu zilizopita. Hata hivyo shirika hilo limesema misaada hiyo ni chini ya misaada yote inayohitajika. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kiutu na masuala ya dharura OCHA limesema licha ya kiwango kidogo, bidhaa za misaada zilizopo zitakuwa na jukumu muhimu katika kuimarisha huduma ya afya mjini Gaza.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW