1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Utawala wa sheriaUganda

Onyo: Muswada Uganda watishia uchumi na misaada

29 Aprili 2026

Benki ya Dunia yaonya kusitisha shughuli Uganda iwapo muswada wa ulinzi wa taifa utapitishwa, huku Benki Kuu ikisema unaweza kudhoofisha uchumi na kuzuia upatikanaji wa fedha za kigeni.

Uganda Kampala 2024 | Polizei riegelt Parlament vor geplanter Anti-Korruptions-Demonstration ab
Picha: Badru Katumba/AFP/Getty Images

Benki ya Dunia imeonya kuwa itasitisha uhusiano na shughuli zake nchini Uganda ikiwa muswada wa ulinzi wa taifa unaojadiliwa sasa utapitishwa kuwa sheria.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, sheria inayopendekezwa kuhusu udhibiti wa mtiririko wa fedha za kigeni itaifanya ishindwe kuendelea kutoa ufadhili kwa serikali na sekta binafsi bila kukiuka sheria hiyo.

Hali hiyo inaweza kulazimisha Benki ya Dunia kusitisha kabisa ushirikiano wake na taasisi zote nchini humo ili kuepuka kuvunja sheria.

Wakati huo huo, Benki Kuu ya Uganda imeonya kuwa kupitishwa kwa muswada huo kunaweza kuathiri vibaya uchumi wa nchi.

Gavana wa benki hiyo, Michael Atingi-Ego, alisema hatua hiyo inaweza kuzuia upatikanaji wa fedha za kigeni zinazohitajika kulipia madeni na kuagiza bidhaa kutoka nje.

Bunge la Uganda linajadili muswada wa Ulinzi wa taifa kwa kasi ambayo imewashtua wengi, hasa kutokana na utata unaogubika vipengele kadhaa vya Muswasa huo.Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Hofu ya kudorora kwa uchumi

Atingi-Ego aliiambia kamati ya bunge kuwa sheria hiyo inaweza kudhoofisha mifumo ya ukuaji wa uchumi na kurudisha nyuma maendeleo kwa hadi miaka 30.

Uganda inategemea kwa kiasi kikubwa fedha za kigeni kwa ajili ya biashara ya kimataifa na huduma za kifedha, hivyo mabadiliko hayo yanaweza kuwa na athari kubwa.

Muswada huo unalenga kuweka udhibiti mkali juu ya mtiririko wa fedha za nje kwa madai ya kulinda maslahi ya taifa.

Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa hatua hiyo inaweza kuathiri uwekezaji na mahusiano ya kimataifa.

Muswada huo umekuja baada ya Rais Yoweri Museveni kushinda muhula wa saba wa miaka mitano, akitarajia kuapishwa mwezi Mei, 2026.Picha: SIMON MAINA/AFP/Getty Images

Upinzani kutoka kwa wadau

Muswada huo pia umepingwa na makundi ya kiraia, viongozi wa kidini na wanaharakati wa haki za binadamu.

Wakosoaji wanasema unampa mamlaka makubwa waziri wa mambo ya ndani kudhibiti fedha za kigeni na unaweza kuwaweka raia, hasa walioko nje ya nchi, katika hali ya sintofahamu kuhusu uraia wao.

Aidha, raia wanaopokea fedha kutoka nje bila idhini maalum wanaweza kutambuliwa kama "mawakala wa kigeni,” hatua inayozua wasiwasi mkubwa.

Waandishi wa habari pia wanaweza kuathiriwa, kwani muswada huo unapendekeza kudhibiti taarifa zinazochukuliwa kuwa na ushawishi wa kigeni.

Baadhi ya wakosoaji wanaamini Muswada huo unalenga kumvunja nguvu mpinzani mkuu wa utawala wa Rais Yoweri Museveni, Bobi Wine, anaehojiwa katika picha hii.Picha: Ronka Oberhammer/DW

Shinikizo la kupitishwa haraka

Licha ya utata huo, bunge la Uganda linaonekana kushinikizwa kupitisha muswada huo haraka kabla ya kumalizika kwa muda wake wa sasa.

Inaripotiwa kuwa bunge lina siku chache tu kukamilisha mchakato huo, hali inayozua maswali kuhusu muda mfupi wa mjadala kwa sheria yenye athari kubwa.

Mjadala unaendelea huku wadau wakitaka uchunguzi wa kina zaidi kabla ya uamuzi wa mwisho kufanywa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW