Open Doors: Mateso ya Wakritu yaongezeka duniani
13 Januari 2021Ripoti hiyo inaitaja hali kuwa mbaya zaidi nchini Nigeria na mataifa mengine ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara, ambapo kati ya visa 4761 vilivyoorodheshwa vya mauaji ya waumini wa dini hiyo, asilimia 91 vilikuwa barani Afrika, huku Nigeria pekee ikichangia visa 3530.
Markus Rohe, mkuu wa shirika la Open Doors nchini Ujerumani, anasema sababu kuu ni kwamba makundi ya itikadi kali yanalenga kuanzisha utawala wa Khalifa, na anazungumzia pia ombwe la kimamlaka kutokana kukithiri kwa rushwa.
"Boko Haramu na wafugaji wa kabila la Fulani wanahusika na mauaji ya Wakristu wengi wanapovamia na kushambulia vijiji vya wakristu kila mahala. Tukio la karibuni zaidi ni la Desemba 24. Hilo lilikuwa kundi la Dola la Kiislamu katika Afrika Magharibi. Makanisa yalichomwa moto, wakristu watano wakatekwa na kuuawa, na hayo yalifanyika mbele kamera na chaneli ya habari ya IS," alisema Rohe.
Kiongozi huyo wa shirika la Open Door anakosoa ukimya wa Ulaya kuhusiana na vurugu hizo barani Afrika. Anasema hata baada ya kurekodiwa kwa visa vya mauaji ya zaidi ya watu 3500 nchini Nigeria, hakujawa na kauli zozote kutoka jamii ya kimataifa.
Viongozi wa Korea Kaskazini, China waabudiwa kama Mungu
Ingawa ripoti za mashambulizi mabaya zaidi dhidi ya Wakristu zinatokea Afrika, Ripoti ya Open Doors inaiorodhesha Korea Kaskazini katika anfasi ya kwanza kwa mara ya 20 mfululizo. Himaya tawala ya familia ya Kim inajiruhusu kuabudiwa kama Mungu, inasema ripoti hiyo. Mamia kwa maelfu ya Wakristu wanalaazimishwa kufanya kazi ngumu kwenye makambi gerezani.
Mataifa yanayofuatia katika orodha hiyo ni Afghanistan, Somalia, Libya, Pakistan, Eritrea ambayo yaliorodheshwa pia mwaka uliyopita. Lakini ripoti hiyo inaainishwa mabadiliko chanya nchini Sudan, kufuatia kuondolewa kwa rais Omar al-Bashir, na kuwekwa kwa mifumo ya kisheria inayoruhusu uhuru wa kuabudu nchini humo.
Ripoti hiyo inachora taswira ya rais wa China Xi Jinping katika nafasi sawa na kiongozi wa Korea Kaskazini Kima Jong Un. Yeyote anamuweka Mungu juu ya Xi laazima ategemee adhabu, linasema shirika hilo la misaada kuhusu kiongozi huyo wa China na mkuu wa chama tawala cha Kikomunisti. Katika faharasi ya Open Doors, China imepanda kutoka nafasi ya 23 hadi 17.
Lakini ripoti hiyo haitaji hali mbaya wanayopitia watu wa jamii ya Uighur, ambao mamia kwa maelfu wamefungwa katika kambi na kufanyishwa kazi za laazima. Shirika hilo linalitaja janga la virusi vya corona kama kichocheo cha madhila ya waumini wa kikristu ambalo linasababisha kuongezeka kwa shinikizo - barani Afrika na pia Asia.
Chanzo: DW