Operesheni Atlanta yaanza mashambulizi ndani ya Somalia
15 Mei 2012Kamanda wa maharamia hao ameliambia shirika la habari la AP kuwa mashambulizi hayo ya ndege yaliyofanywa na jeshi la majini la Umoja wa Ulaya linalofanya doria kwenye Bahari ya Hindi yameharibu boti, ghala la mafuta na ghala la silaha.
Bile Hussein amekiri kwamba mashambulizi hayo katika Handulle mkoani Mudug litarejesha nyuma operesheni zao. Kijiji hicho kiko umbali wa kilomita 18 kaskazini mwa mji wa Hardhere, ambao ni kitovu cha shughuli za uharamia.
Mapema Umoja wa Ulaya ulisema kwamba kikosi chake cha majini kimefanya mashambulizi hayo ya kwanza kabisa kwa njia ya anga kwa kutumia helikopta na ndege za kijeshi.
"Operesheni ya Umoja wa Ulaya kupambana na uharamia, operesheni Atlanta, asubuhi hii imeshambulia vituo vinavyowawezesha maharamia kufanya kazi zao ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi wa baraza la mawaziri la Umoja wa Ulaya. Mashambulizi haya yalisababisha boti kubaribiwa." Amesema Timo Lange wa kitengo cha habari cha Operesheni Atlanta yenye makao yake makuu Northwood, Uingereza.
Haramia mwengine wa Kisomali aliyejitambulisha kwa jina moja la Abdi, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa helikopta moja ililishambulia eneo la pwani la Hardhere, lakini hakukuwa na madhara yoyote kwa raia.
Abdu amesema kwamba wakati helikopta hiyo ilipokuja kuwashambulia walikuwa wamekaa nje kwenye ufukwe. "Tulikimbia tu na wala hatukurejesha mashambulizi." Amesema Abdi.
Mwezi Machi Umoja wa Ulaya ulitanua operesheni yake ya kupambana na maharamia katika pwani ya Somalia kuishia hadi mwishoni mwa mwaka 2014, na kuongeza eneo la kufanyia operesheni hiyo, sasa likijumuisha ukanda wa pwani wa Somalia.
Kabla ya mashambulizi ya leo, operesheni Atlanta ilikuwa ikifanya kazi ndani ya bahari tu, bali uamuzi wa kuingia ndani ya ardhi ya Somalia unamaanisha sasa kikosi hicho cha Umoja wa Ulaya kinaweza kuyalenga maghala ya silaha na zana zinazotumiwa na maharamia katika matayarisho ya operesheni zao.
Licha ya kufanikiwa kuzuia mashambulizi katika Ghuba ya Aden, majeshi ya kimataifa yamekuwa yakipata tabu kuudhibiti uharamia katika Bahari ya Hindi na ya Arabuni kutokana na upungufu wa rasilimali na ukubwa wa eneo husika.
Maharamia wameweza kujikusanyia mamilioni ya dola kama fedha za kuzikombolea meli wanazozikamata katika miaka ya hivi karibuni, katika ule unaoitwa uharamia wa kimataifa uliopangika vyema.
Utafiti uliochapishwa mwanzoni mwa mwaka huu na Wakfu wa One Earth Future unaonesha kuwa uharamia wa Somalia uliugharimu uchumi wa dunia kiasi ya dola bilioni 7 za Kimarekani kwa mwaka jana peke yake, ambapo fedha zilizolipwa kukombolea meli na mabaharia zilifikia dola milioni 160.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters/DPA
Mhariri: Othman Miraji