"Operesheni Mushtarak" yaendelea Afghanistan
15 Februari 2010Matangazo
Kwa mujibu wa duru za kijeshi za Afghanistan, majeshi yanayoongozwa na Marekani yamedhibiti takriban eneo zima lililokuwa chini ya Wataliban, baada ya kuwa na mapigano makali kutoka nchi kavu na angani. Hadi hivi sasa raia 12 wa Afghanistan na wanajeshi 2 wa NATO wameuawa katika eneo la Marjah wilayani Helmand katika operesheni inayoitwa "Operesheni Mushtarak" yaani operesheni ya pamoja kwa lugha ya Dari. Wanajeshi wengine 5 wa NATO waliuawa kwengineko kusini mwa Afghanistan. Jenerali Lashkar Gah wa Afghanistan alipozungumza na shirika la habari la AFP alisema takriban sehemu zote zilizolengwa katika maeneo ya Marjah na Nad Ali katika Wilaya ya Helmand yamedhibitiwa na vikosi vya pamoja na wanamgambo 27 wameuawa. Hata hivyo msemaji wa majeshi ya Marekani amesema kuwa wamekutana na upinzani mkali katika baadhi ya vijiji ukingoni mwa Marjah. Katika maeneo hayo majeshi ya pamoja yanashambuliwa na Wataliban kwa risasi na magruneti yanayorushwa kwa makombora. Wakati huo huo, maafisa wa Afghanistan wanasema, serikali imekaa tayari kwenda katika maeneo yaliyokombolewa na inatazamia kuanzisha huduma za kijamii na usalama ili kuhakikisha kuwa Wataliban hawatorejea tena. Ili kuweza kupata imani ya raia katika maeneo hayo, operesheni hiyo ya kijeshi inapaswa kuepusha vifo vya wakaazi kama iwezekanavyo. Siku ya Jumapili NATO ilikiri kuwa kwa makosa, makombora yao yaliangukia eneo la makaazi na yalisababisha vifo vya Wafghanistan 12 katika eneo la Marjah. Kamanda wa Marekani nchini Afghanistan Jemadari Stanley McChrystal ameomba msamaha kwa vifo hivyo wakati mshauri wa masuala ya usalama wa taifa wa Marekani James Jones akisema kuwa operesheni hiyo inaendelea vizuri. Kwa upande mwingine, taarifa iliyotolewa na Taliban imemnukulu Mullah Abdul Rezaq Akhund akiilani operesheni hiyo kama ni njama ya kueneza propaganda. "Operesheni Mushtarak" inaendeshwa na wanajeshi 15,000 wa Marekani, NATO na Afghanistan tangu siku ya Jumamosi na ni mtihani wa kwanza kwa mpango wa Rais wa Marekani Barack Obama kupeleka wanajeshi 30,000 zaidi nchini Afghanistan. Lengo ni kuyadhibiti maeneo yaliyotekwa na wanamgambo wa Taliban na kurejesha serikali ya kiraia katika maeneo hayo. Mwandishi:Prema Martin/AFP Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed
Matangazo