1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Operesheni ya Israel yaua Wapalestina 300 Khan Younis

30 Julai 2024

Mamlaka za Gaza zimesema siku ya Jumanne kuwa karibu Wapalestina 300 wameuawa kufuatia operesheni ya jeshi la Israel iliyoanza Julai 22 huko Khan Younis.

Wakazi wa Gaza wakirejea makwao katika mji uliosalia kuwa magofu wa Khan Younis
Wakazi wa Gaza wakirejea makwao katika mji uliosalia kuwa magofu wa Khan YounisPicha: Omar Ashtawy/apaimages/IMAGO

Wakati operesheni ya jeshi la Israel iliyoanza mwanzoni mwa wiki iliyopita ikikamilika huko Khan Younis ambao ni mji wa pili kwa ukubwa katika Ukanda wa Gaza, Msemaji wa Shirika linalohusika na ulinzi wa raia wa  Gaza  Mahmud Bassal amesema hivi leo kwamba operesheni hiyo ilisababisha vifo vya takriban watu 300, na kwamba miili mingine ilipatikana ikiwa katika hali mbaya.

Hata hivyo jeshi la Israel limedai kuwa limefanikiwa kuwaangamiza "magaidi" wapatao 150 katika operesheni hiyo iliyoanzishwa Julai 22 na kwamba waliharibu pia mahandaki ya magaidi, vituo vya kuhifadhia silaha na miundombinu kadhaa. Kwa sasa, wakazi wa Khan Younis wameanza kurejea makwao katika mji uliosalia kuwa magofu kwa kiasi kikubwa.

Hali ya kibinaadamu inazidi kuwa mbaya huko Gaza

Kunashuhudiwa kwa sasa katika Ukanda wa Gaza uhaba mkubwa wa bidhaa muhimu kama chakula, maji safi na dawa. Shirika la Afya Duniani WHO limesema kuna uwezekano mkubwa kuwa idadi kubwa ya wakazi wa Gaza wana ugonjwa wa polio.

Wapalestina wakipokea msaada wa chakula huko GazaPicha: Hatem Khaled/REUTERS

Shirika la kimataifa la kuwahudumia watoto UNICEF limeonya kuhusu ugumu wa watoto wa Kipalestina kupata maji safi na chanjo. James Elder,  ni msemaji wa UNICEF:

"Bila ya maji safi, watoto au familia zilizo katika mazingira magumu hulazimika kutumia maji yasiyo salama, na hivyo kuwaweka katika hatari zaidi ambazo tumezishuhudia mara kwa mara, siku baada ya siku huko Gaza, ambazo ni upungufu wa maji mwilini, utapiamlo na magonjwa.”

Soma pia: UN: Vita vya Gaza vimewaathiri mno wanawake na watoto

Vita vya Gaza hadi sasa vimekwishasababisha vifo vya watu 39,400, hii ikiwa ni kulingana na wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas.

Israel yataka Uturuki iondolewe kwenye NATO

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Katz amezitolea wito nchi za Magharibi kuiondoa Uturuki kwenye Jumuiya ya Kujihami ya NATO akisema nchi hiyo imetoa vitisho vya wazi kwa Israel na kwamba inashirikiana na Iran na kuwahifadhi magaidi wa Hamas.

Katz ambaye amemfananisha Erdogan na rais wa zamani wa Iraq Saddam Hussein, amesema Uturuki imekiuka kwa kiasi kikubwa kanuni za NATO kwa kutishia bila uchochezi wowote, kuivamia nchi ya kidemokrasia yenye mfumo wa kimagharibi.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: DHA

Mapema wiki hii, rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alitishia kuingilia kati mzozo wa Gaza na kusema Uturuki ingeliweza kuingia hadi Israel kama ilivyofanya kwenye mizozo ya Libya na Nagorno-Karabakh ili kuizuia Israel kuendeleza kile alichokiita "matendo ya kipuuzi ya Israel huko Gaza".

Hayo yakiarifiwa  mzozo kati ya Israel na kundi la Hezbollah  pia unatokota. Israel imesema hivi leo kuwa imeshambulia usiku wa kuamkia leo maeneo 10 ya kundi hilo kusini mwa Lebanon na kumuua mpiganaji mmoja. Uingereza imewataka raia wake kuondoka mara moja nchini Lebanon. Jumuiya ya kimataifa imetoa miito ya kuepusha kuutanua mzozo huo na kulitumbukiza eneo zima la Mashariki ya Kati kati vita vya kikanda.

(Vyanzo: APE, RTRE, DPAE, AFP)